October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Madiwani Moshi wadaiwa kuunda mtandao wa kula rushwa, kuruhusu ujenzi holela

Spread the love

NI KASHFA! Ndivyo unavyoweza kuelezea kile kilichojiri mkoani Kilimanjaro katika Manispaa ya Moshi mjini ambapo madiwani wa Kata nne za manispaa hiyo, wamedaiwa kuunda mtandao wa kukusanya fedha kutoka kwa watu au wafanyabiashara wanaotaka kukarabati na kujenga nyumba za chini kinyume na taratibu za mwongozo wa mpango mji unaotumika sasa kwenye mji huo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hatua hiyo imekuja baada ya mwaka 2001, Manispaa hiyo kupitisha mwongozo unaotaka ujenzi au ukarabati wa nyumba zozote ikiwamo za biashara uanzie ghorofa mbili kwenda juu na kupiga marufuku ujenzi au ukarabati wa nyumba za chini hususani katika kata za Bondeni, Kiusa, Korongoni, Mawenzi na Miembeni.

Mafundi wakiendelea na ujenzi wa nyumba ya chini ujenzi ambao kwa Manispaa ya Moshi umezuiwa

Hata hivyo, madiwani hao kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bashiri Tassama (kata ya Kiusa), Masiu Kilusu (Bondeni), Heavenlight Kiondo (Korongoni) na Mohamed Mushi (Miembeni) wamedaiwa kushirikiana na Meya wa Manispaa hiyo, Zuberi Kidumo ambaye pia ni Diwani wa kata ya Njoro kuendeleza ujenzi holela wa nyumba za chini.

Madiwani hao wanadaiwa kuchukua kiasi cha Sh milioni 6 hadi 10 kutoka kwa watu wenye uhitaji wa kufanya ukarabati au kujenga nyumba za chini katika kata zao jambo ambalo limedaiwa kuwanyima haki wananchi wa kawaida wenye uhitaji wa kufanya ukarabati wa nyumba zao kwa sababu tu hawana fedha za kuwahonga.

WANATUMIKAJE?

Akizungumza na Raia Mwema kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa wawakilishi wa kampuni ya Barack Printers Ltd. ambayo ilishinda zabuni ya ukusanyaji ushuru wa aina mbalimbali ikiwamo majengo katika eneo hilo, alisema tangu walipoanza kazi hiyo Agosti mwaka huu, kikwazo kikubwa kwao ni madiwani.

Alifafanua kuwa madiwani hao wa kata za Kiusa, Bondeni na Korongoni, huwazuia wananchi wanaotaka kukarabati nyumba za chini na kuwataka kuzingatia mwongozo huo unaowataka kutofanya badiliko lolote la makazi yao zaidi ya ujenzi wa ghorofa.

“Wale ambao wenye fedha, ndio wanaowahonga madiwani hao ambapo madiwani huwasaidia kupata kibali cha ujenzi kutoka Manispaa na kuendelea na ujenzi.

Kibao cha maelezo ya ujenzi wa nyumba ya ghorofa mbili kikiwa kimebandikwa katika eneo la Kata ya Bondeni. Nyumba iliyojengwa hapo ni ya chini na baada ya kelele za wananchi kibao hicho kiling’olewa.

“Tunapokuja sisi kukagua ujenzi unaoendelea na kubaini wampeta kibali kinyume cha taratibu tukiwapa ‘stop order’ ndipo madiwani hujitokeza kutuzuia kutekeleza wajibu wetu kwa sababu wao ndio waliopitisha mwongozo huo na wanafahamiana na watu manispaa, basi inatuwia vigumu kuendelea kupambana nao,” alisema.

Alitolea mfano kuwa kuna nyumba iliyojengwa katika Kata ya Bondeni, ambapo madiwani hao walipiga kambi kwa zamu kusimamia ujenzi huo hadi nyumba hiyo ya chini ilipokamilika.

WANANCHI HAWA HAPA

Baadhi ya wananchi waliozungumzia kadhia hiyo, walisema kinachoendelea sasa ni kwamba mwenye fedha ndiye anayeruhusiwa kujenga au kukarabati nyumba ya chini na asiye na haruhusiwi.

Mmoja wa wakazi hao wa mtaa wa Uswahili kata ya Kiusa, Hassan Mzava alisema utaratibu huo wa ujenzi wa ghorofa ulipopitishwa, kwa pamoja walifurahia kwa sababu nao walitaka kuona mji wa Moshi unajengwa maghorofa na kupangika vizuri kama jiji.

“Kilichotushangaza kuona maghorofa hayajengwi, kinachojengwa ni nyumba za chini tena, jirani kwangu kuna bango liliwekwa kwamba ujenzi ni wa ghorofa mbili lakini baadae ikabainika ni nyumba ya chini iliyojengwa.

“Hayo yanatokea wakati  sisi tuliomba kufanya ukarabati wa bati kwenye nyumba yetu tukanyimwa. Tukamuendea diwani wetu wa kata ya Kiusa atusaidie akataka tumpe Sh milioni nane, tukamgomea.

“Waliotoa milioni 10 wameruhusiwa kujenga, tulimfuata hadi Meya wa Moshi naye hakutuelewa kabisa,” alisema.

Madai hayo yaliungwa mkono na mkazi mwingine wa eneo hilo aliyefahamika kwa jina la Issa Maulid ambaye alisisitiza kuwa ni kweli kwamba bila kuwa na hela huwezi kupatakibali cha ujenzi.

KAMPUNI YA MEYA YATAJWA, NYUMBA YAJENGWA, KIBAO CHANG’OLEWA

Wakati tuhuma hizo zikimiminika kwa madiwani hao, kwa upande wa Kata ya Bondeni, nako kumebainika kujengwa nyumba ya chini lakini ili kuwahadaa wananchi, pakawekwa kibao cha maelezo ya ujenzi kuwa ujenzi huo ni wa ghorofa mbili za biashara.

Hata hivyo, uchunguzi wa Raia Mwema ulibaini kuwa nyumba hiyo ni ya chini, kwani baada ya kufikia kwenye hatua ya kuezekwa na wananchi kupiga kelele kuhusu ujenzi huo, kibao hicho kilichokuwa kimewekwa ramani ya ujenzi wa nyumba ya ghorofa mbili, killing’olewa usiku wa manane.

Aidha, katika kibao hicho cha maelezo, pia ilidaiwa kuwa kampuni ya ukandarasi aliyekuwa akisimamia ujenzi huo, ni ya Meya wa Moshi.

Nyumba hiyo iliyojengwa na mfanyabiashara Amani Iddi Mushi, imejengwa katika Plot no. 4 block ‘S’ eneo la Bondeni Moshi.

MADIWANI WAFUNGUKA

Wakizungumza na Raia Mwema kwa nyakati tofauti, madiwani hao walikanusha madai hayo ya kuchukua fedha kwa watu ili wapate idhini ya kujenga nyumba za chini katika eneo hilo.

Diwani wa Kata ya Bondeni, Masiu Kilusu ambako ndiko kulikojengwa nyumba ya chini wakati ramani ilionesha panajengwa  ghorofa, alisema suala la mjenzi kubadilisha ramani halimuhusu.

“Kama kulikuwa na ramani ya ghorofa alafu akabadilisha akajenga nyumba ya chini… shauri yake! Kama ameharibu atajijua mwenyewe, mimi siwezi kupingana na serikali,” alisema.

Kuhusu suala la kuchukua fedha kwa wafanyabiashara hao ili wapate idhini ya ujenzi, Diwani huyo alisema sio yeye anayepaswa kutoa vibali vya ujenzi, hivyo suala halina ukweli wowote.

“Hakuna diwani yeyote anayeweza kutoa maelekezo. Kama kuna tatizo kwamba mtu anataka kurepear bati, kuna taratibu zinamruhusu kufanya hivyo, yaani unatakiwa kufanya marekebisho madogo mathalani kubadilisha bati moja au mbili, lakini si nyumba nzima,” alisema.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kiusa, Bashiri Tassama alikanusha kuchukua fedha kwa wananchi wanaotaka kujenga nyumba za chini na kuongeza kuwa hivi karibuni wamepitisha mwongozo mpya utakaowaruhusu wananchi kufanyia ukarabati au kujenga nyumba zao bila bughdha.

“Kuhusu suala la vibali, hilo silifahamu, waulize watu wa vibali, ni suala la utumishi,” alisema na kuongeza kuwa tuhuma hizo ni za watu wanaotaka kumlisha maneno ya uongo.

Diwani wa kata ya Korongoni, Heavenlight Kiondo aligoma kuzungumzia tuhuma hizo kwa madai kuwa hilo ni suala linalopaswa kuzungumzwa na viongozi wa Halmashauri ilihali naye Diwani wa Kata ya Miembeni, Mohamed Mushi naye simu yake iliita bila kupokewa.

MEYA AFUNGUKA, AANIKA MIKAKATI

Akizungumzia tuhuma hizo, Meya wa Manispaa hiyo, Zubeir Kidumo alikana kuungana na mtandao wa madiwani hao ili kuchukua fedha kutoka kwa wananchi wanaotaka kujenga nyumba za chini.

Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa taarifa za baadhi ya madiwani kuchukua fedha kutoka kwa wananchi ili kuwakingia kifua wajenge nyumba za chini.

Alisema kutokana na hali hiyo, tayari baraza la madiwani limekaa na kupitisha rasimu ya mwongozo mpya wa ujenzi katika Manispaa hiyo ya Moshi.

Alisema mwongozo huo ambao, sasa umepelekwa kwa Ofisi za Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) ili kupata baraka za waziri, sasa zitatoa uhuru kwa mwananchi kukarabati au kujenga nyumba ya chini au ghorofa kwa utaratibu maalumu.

“Muongozo wa awali ulikuwa unatoa mwanya kwa madiwani na wajanja wa mjini kuwaibia wananchi fedha zao, na wengi wao kwa kutojitambua wamewahonga fedha ili wajenge au kukarabati nyumba zao.

“Tumeliona hili ndio maana utaratibu huu mpya, tutautangaza baada ya kupata baraka za TAMISEMI, kwamba hakuna atakayezuiwa tena kujenga au kukarabati nyumba yake, ila atapewa kibali maalumu.

“Lengo ni kuupendezesha mji wa Moshi na sio kubaki kama maghofu, hata Kariakoo haikujengwa kwa siku moja, palikuwa na utaratibu wa namna hii, huyu atakayejenga nyumba ya chini leo, kesho atajenga ghorofa mbili na kuendelea,” alisema.

Kuhusu kampuni yake inayodaiwa kushiriki ujenzi huo wa holela, Meya huyo alisita kukubali au kukataa lakini akakiri kumiliki kampuni ya ujenzi ambayo inapewa zabuni za ujenzi na watu wa kawaida na si kutoka serikalini jambo ambalo si kinyume cha sheria.

“Sasa mimi kama nina kampuni yangu, nimepewa tenda nijenge na rafiki yangu nitaacha kujenga nimwambie mimi ni meya siruhusiwi? Hili ni jambo ambalo linafahamika na sizuiwi kufanya biashara hiyo,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu nyumba ya chini aliyoijenga katika kata ya Bondeni licha ya kibao cha maelezo ya ujenzi kuonesha kuwa pangepaswa kujengwa ghorofa, Meya huyo alisisitiza kuwa akishapewa kazi na mteja, anayeamua kubadilisha ramani ya ujenzi ni mteja mwenyewe, yeye kazi yake ni kujenga tu.

Aidha, Mhandisi wa Manispaa hiyo ya Moshi, Richard Sanga licha ya kukiri kuwa tayari wamesimamisha ujenzi wa nyumba hiyo ya chini katika kata ya bondeni, alisita kufafanua namna wanavyotoa vibali vya ujenzi kiholela.

“Kuhusu suala la utoaji wa vibali njoo ofisi upate ufafanuzi, kuna utaratibu maalumu,” alisema.

DED APATA KIGUGUMIZI

Aidha, Raia Mwema lilizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Rashid Gembe ambaye baada ya kuelezwa tuhuma zinazowakabili madiwani pamoja na meya wa manispaa hiyo, aliomba kutafutwa baadae kwani hayupo katika mazingira mazuri ya kuzungumzia tuhuma hizo.

 

error: Content is protected !!