Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Cuba zimesaini hati za makubaliano ya kushirikiana katika sekta ya elimu ya juu kwa kubadilishana wakufunzi na wanafunzi, kufundisha lugha ya kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana nchini Cuba pamoja na kutengeneza kamusi ya Kiswahili na Kihispaniola. Anaripoti Mwandishi Wetu.
Makubaliano hayo yamesainiwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba iliyofanyika Jijini Havana na kushuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Cuba, Salvador Valdes Mesa.

Makubaliano hayo yamesainiwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Stephen Byabato kwa niaba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba, Dk. Walter Garcia.
Mbali na Makubaliano ya elimu, makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam na Chuo Kikuu cha Havana ambapo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kiliwasilishwa na Makamu Mkuu wa chuo hicho Prof. William Anangisye wakati Chuo Kikuu Cha Havana kiliwasilishwa na Prof. Miriam Garcia
Katika makubaliano hayo Tanzania na Cuba zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kupitia wahadhiri, wanafunzi, tafiti, sayansi, teknolojia, kufundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana na kutengeneza kamusi ya lugha ya Kiswahili na Kispaniola ili kusambaza matumizi ya lugha ya kiswahili nchini Cuba na nchi nyingine zinazozungumza lugha ya kihuspaniola.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole amesema Ubalozi wa Tanzania Havana unajivunia kusainiwa kwa makubaliano hayo ambayo yanatoa mwongozo maalum wa jinsi ya kutekeleza mpango wa kufundisha lugha ya Kiswahili nchini humo.
“Haya ni mafanikio makubwa kwetu, Ubalozi wa Tanzania Havana unajivunia kusainiwa kwa makubaliano haya, sasa yatatoa mwongozo maalum utakaowezesha taasisi husika za elimu ya juu kutekeleza kikamilifu mpango wa kusambaza na kueneza lugha ya Kiswahili nchini Cuba,” alisema Balozi Polepole.
Makubaliano mengine yaliyosainiwa ni kati ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknojia na Wizara ya Elimu ya Juu ya nchini Cuba ambayo yatawezesha ubadilishanaji wa wanafunzi, wahadhiri na watafiti katika eneo la sayansi na teknolojia ili kuwawezesha wahusika kubadilishana ujuzi na uzoefu katika maeneo hayo na hivyo kuleta tija na ufanisi kwa pande zote mbili.
Makubaliano hayo yamesainiwa katika hafla ya uzinduzi wa Ubalozi wa Tanzania Cuba iliyofanyika Jijini Havana tarehe 14 Septemba 2023 na kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi na Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Valdes Mesa na Jumuiya ya wana Diplomasia waliopo jijini Havana.
Leave a comment