Thursday , 9 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kikwete: Amani itawezesha nchi za SADC kujiamini, kusimamia haki
Habari za Siasa

Kikwete: Amani itawezesha nchi za SADC kujiamini, kusimamia haki

Spread the love

Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema amani na usalama ni maneno yenye dhana pana tofauti na watu wengi wanavyoelewa kuwa amani na usalama ni kuwa huru katika migogoro inayotumia silaha. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Kikwete ametoa kauli hiyo jana Jumamosi wakati anawasilisha mada kuhusu amani na usalama kama kigezo cha msingi cha kufikia maendeleo ya kweli Kusini mwa Afrika.


Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete (mwenye tai nyekundu) akiwa na ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika mhadhara wa umma ambao aliwasilisha mada kuhusu amani na usalama kama msingi wa kufikia maendeleo ya kweli katika nchi za Kusini mwa Afrika

Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la Wazee wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) aliwasilisha mada hiyo kwenye Chuo cha Diplomasia cha Angola ikiwa ni moja ya matukio ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulioanza tarehe 8 Agosti 2023 kwa ngazi ya maafisa waandamizi na utahitimishwa na Mkutano wa Marais utakaofanyika tarehe 17 Agosti 2023.

“Amani na Usalama ni dhana pana inayojumuisha mambo mengi kama vile elimu, afya na ustawi wa jamii”,  Kikwete alisema.

Alieleza kuwa amani na usalama ni msingi wa maendeleo Kusini mwa Afrika na itakapokosekana mahali popote pale, watu wasitarajie kupata maendeleo.

Alitoa mfano wa nchi zilizokuwa na migogoro ya kisiasa kwa muda mrefu kama Angola na Msumbiji namna zilivyoathirika kiuchumi hadi hapo ufumbuzi ulipopatikana.

Alisema, utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani na mazingira tulivu yaliyopo hivi sasa, imeshuhudiwa mataifa mengi ya kusini mwa Afrika yanapiga hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aliongeza kuwa taifa lisilokuwa na amani haliwezi kufanya biashara; haliwezi kuvutia uwekezaji kutoka nje na hata ndani ya nchi; haliwezi kujenga miundombinu kama ya Barabara, shule na vituo vya afya kwa sababu fedha zote ambazo Serikali inazipata, zinatumika kununua silaha kwa ajili ya kujilinda.

Alihitimisha mada yake kwa kusisitiza umuhimu wa nchi za SADC zishirikiane kuhamasisha amani katika nchi zao.

“Amani itaziwezesha Serikali za nchi hizo kujiamini na hatimaye kuwa na utawala bora, utawala wa sheria na kutoa haki kwa watu wote,” amesema.

Viongozi wengine mashuhuri walioungana na Rais Kikwete kuwasilisha mada katika Mhadhara huo wa Umma ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Msumbiji, Luisa Diogo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zamani wa Angola, Balozi Joao Bernardo de Miranda ambao mada zao zilihusu miundombinu inayohitajika kuunganisha nchi za SADC na hali ya sasa ya dunia na athari zake kwa nchi za SADC.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yapunguza kodi ya makampuni kwa 20%

Spread the loveSERIKALI imepunguza kodi ya makampuni kwa asilimia 20, kutoka asilimia...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu, Halima Mdee hapatoshi

Spread the loveVITA ya maneno kati ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Madiwani Msalala wampa tano DED kwa kuongeza mapato

Spread the loveMKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, mkoani Shinyanga, Khamis...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kimbunga Hidaya chaua 5, kaya 7,027 zikikosa makazi

Spread the loveSERIKALI imetoa tathmini ya athari za kimbunga Hidaya, kilichotokea tarehe...

error: Content is protected !!