Thursday , 9 May 2024
Home Kitengo Maisha Afya Haya ndio maboresho ya kitita cha mafao – NHIF
Afya

Haya ndio maboresho ya kitita cha mafao – NHIF

Spread the love

KATIKA kuboresha huduma za matibabu nchini na kuendana na bei halisi ya utoaji wa huduma hizo, Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF) imejipanga kufanya maboresho ya kitita cha mafao katika maeneo mbalimbali. Anaripoti Gabriel Mushi…(endelea).

Kitita cha mafao cha msingi ni ujumuishaji wa huduma zote muhimu ambazo kila mgonjwa atastahili kulingana na viwango vya michango vilivyowekwa katika kanuni na kadri waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya atakavyokuwa akiboresha kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam.

Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika kikao kazi kilichofanyika jana tarehe 18 Desemba 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga amesema maboresho hayo yanakwenda kuleta ahueni kwa wanachama na wadau kwa ujumla ili kuhakikisha wanatoa huduma bora.

Amesema maboresho hayo yanakwenda kuongeza jumla ya dawa 124 kutoka katika Orodha ya Dawa Muhimu ya Taifa (NEMLIT), kupunguza gharama za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo, kuondoa changamoto za uandishi wa majina ya baadhi ya vipimo pamoja na kuongeza wigo wa huduma za kibingwa za upasuaji katika hospitali zote za rufaa ya kanda na Taifa.

Konga amesema wameweka usawa wa ada ya kumuona daktari pamoja kutambua uwepo wa kada ya madaktari katika ngazi ya afya ya msingi jambo ambalo litawasaidia watanzania kupata huduma bora kupitia mfuko huo.

Amesema katika maboresho hayo wamejumuisha dawa zenye nguvu na muundo kwa kuzingatia upatikanaji wa dawa katika soko pamoja na mabadiliko katika ngazi za matumizi ya dawa kama ilivyoanishwa mwongozo wa tiba nchini.

Kuhusu huduma ya usafishaji figo, amesema kutokana na maboresho hayo ambayo yanaanza kutumika rasmi tarehe 1 Januari 2024, wagonjwa wa figo ambao walikuwa wakisafishwa damu kwa Sh 240,000, sasa watatumia Sh200,000.

“Katika huduma ya upasuaji na vipimo tutafanya maboresho ambayo yamelenga kwenda sambamba na mapitio ya gharama halisi na uchambuzi wa uhalisia wa bei katika soko” amesema Konga.

Amesema watazingatia mambo muhimu katika maboresho hayo ikiwemo kufanya utafiti wa gharama halisi za matibabu katika soko pamoja na kushirikisha wadau wa sekta binafsi kwa lengo la kupata maoni, ushauri na mapendekezo kuhusu kitita.

Aidha, amesema katika kudhibiti matumizi wataimarisha utambuzi wa wanufaika katika vituo vya kutolea huduma kwa kutumia alama za vidole pamoja na kuweka “Platform” ya kieletroniki itakayowezesha watoa huduma kubadilisha taarifa za wagonjwa miongoni mwa vituo.

Meneja Uhusiano wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), Anjela Mziray.

Amesema kuwa wameweka utaratibu utakaowezesha wanufaika kuzingatia utaratibu wa rufaa, kuongeza huduma zitakazo hitaji uchangiaji (co- payments) na ukomo wa ugharamiaji kwa baadhi ya huduma za makundi ya wanachama (copping).

“Kutakuwa na mfumo wa utambuzi wa madaktari katika vituo vya kutolea huduma nchini, pia tutachukua hatua stahiki kwa watakaodhibitika kujihusisha na vitendo vya udanganyifu” amesema Konga.

Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo, Afisa wa Habari Mwandamizi Mkuu – Habari Maelezo, Liliani Shirima, amesema ni jambo jema kukutana na makundi muhimu ikiwemo wahariri ambao wanajukumu la kuhabarisha umma pamoja na kutoa elimu.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Jene Mihanji, amesema vyombo vya habari vitaendelea kutoa ushirikiano ili kuhakikisha malengo yanafikiwa.

“Tutaendelea kutoa ushirikiano ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu huduma za NHIF” amesema Mihanji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

AfyaHabari Mchanganyiko

Huduma za kibingwa zazinduliwa katika hospitali za halmashauri 184

Spread the loveSERIKALI imezindua huduma za matibabu za kibingwa katika hospitali 184...

AfyaHabari Mchanganyiko

200 wapimwa afya na GGML katika maonesho ya OSHA

Spread the loveZAIDI ya watu 200 jijini Arusha wamejitokeza kupimwa afya na...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!