December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Gambo amtwisha mizigo ya Arusha Rais Samia

Mrisho Gambo, Mbunge wa Arusha mjini, (Ccm)

Spread the love

 

MBUNGE wa Arusha Mjini nchini Tanzania kupitia chama tawala- (CCM), Mrisho Gambo, amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, atatue changamoto zinazoukabili Mkoa wa Arusha. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Gambo amezifikisha changamoto hizo kwa Rais Samia, leo Jumapili, tarehe 17 Oktoba 2021, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Amri Abein jijini Arusha.

Mbunge huyo wa Arusha Mjini, amemuomba Rais Samia, aondoe zuio la mauzo ya madini ya Tanzania, nje ya Mkoa wa Manyara, akisema zuio hilo limekosesha ajira madalali takribani 3000 wa mkoa huo.

“Arusha na Manyara kihistoria ni mmoja, tumekuwa tukinufaika na madini ya Tanzanite, tumeanzisha masoko ya madini, kuna mawazo yametolewa madini yawe Mirerari peke yake, tunaomba fusra hiyo na watu wa Arusha na sisi tuipate,” amesema Gambo.

Gambo amesema “tunao madalali kama 3,000, tangu tangazo limetoka sasa hivi hawana kazi hawapati madini na mwisho wa siku inasababisha kuchukia Serikali yao. Sababu wewe ni mama, imani yangu utatoa maelekezo ili wahusika wakae wapitie upya ili tulinde madini yetu.”

Mwanasiasa huyo, amemuomba Rais Samia apunguze kodi katika sekta ya utalii, ili watalii wapate nafuu dhidi ya athari zilizotokana na janga la Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19).

Wakati huo huo, Gambo amemuomba Rais Samia, amalize mgogoro kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wananchi wa Kata ya Moshono, ili kunusuru makazi ya wananchi hao ambao wamepewa notisi ya kuondoka.

“Tunaomba rais uingilie kati ili eneo ambalo watu wako wamejenga kwa muda mrefu, waruhusiwe kuendelea na wanajeshi wetu wabaki lakini jeshi wamepewa eneo lingine kubwa zaidi ya hekta 10,” amesema Gambo.

Mbunge huyo wa Arusha Mjini, amemuomba Rais Samia alipatie Jiji la Arusha stendi kubwa ya mabasi, huku akimsihi Serikali ipeleke mikutano mkoani humo kwa ajili ya kuendeleza utalii.

Aidha, Gambo amemuomba Rais Samia akamilishe ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) la Hospitali ya Mount Meru, uliokwama kutokana na ukata wa fedha.

“Tuna changamoto upande wa afya, Mount Meru ina changamoto nyingi kwanza haina ambulance ya uhakika, kuna jengo la OPD complex la ghrofa 14, limekwama mpaka sasa. Limeshaanza msingi mpaka sasa halijaendelea, tusaidie tupate fedha jengo likamilike,” amesema Gambo.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesema, serikali anayoingoza itahakikisha inashughulikia changamoto hizo.

error: Content is protected !!