December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

NMB yamwaga misaada ya mamilioni sekta afya, elimu

Spread the love

 

BENKI ya NMB nchini Tanzania, imehitimisha maadhimisho wiki ya huduma kwa mteja kwa kutumia Sh.180.25 milioni kutoa misaada ya sekta ya elimu na afya katika mikoa mbalimbali nchini ili kuunga juhudi za serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka, wiki ya kwanza ya Oktoba, hutumika kwa kampuni mbalimli kuonesha shughuli zao kwa wateja na kwa mwaka 2021, ilikuwa na kauli mbiu ‘Nguvu ya Huduma.’

Ndani ya kipindi hicho cha wiki moja kuanzia tarehe 3 Oktoba mwaka huu, benki hiyo imetoa misaada hiyo katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Simiyu, Iringa, Rukwa, Mara, pamoja na Kilimanjaro.

Mkoani Dodoma, Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alikabidhi viti 200 na meza 200 kwa ajili ya Shule za Sekondari za Nondwa, Msisi Juu na Bahi za wilaya ya Bahi na Shule ya Sechelela katika Jiji la Dodoma kwa kwa mkuu wa mkoa huo Anthony Mtaka.

Pia, alikabidhi dawati 50 kwa shule ya Msingi Chiguluka, mabati ya kuezekea Sekondari ya Bahi na vifaa vya hospitali kwa zahanati ya Chimendeli na Hospitali ya wilaya Bahi na kuzindua hati ya kiapo cha huduma kwa wateja ikilenga kutoa huduma kwa saa 24.

Akipokea vifaa hivyo, Mtaka alipongeza benki hiyo kwa namna ambavyo imeendelea kutoa msaada unaogusa jamii ya chini akisema alama na mbegu wanayoipanda haitafutika mioyoni mwa watu huku akiiomba kuendelea kuangalia na makundi mengine yenye uhitaji ikiwemo wanawake.

Mkoani Mara, walitoa msaada wa madawati 100 yenye thamani ya zaidi ya Sh.10 milioni kwa shule ya Msingi Kiriba iliyopo halmashauri ya wilaya ya Musoma vijijini.

Msaada huo umesaidia kumaliza kabisa tatizo la upungufu wa madawati, lilokuwa likiikabili shule hiyo kwa muda mrefu na kusababisha baadhi ya wanafunzi kukaa chini wakati wa vipindi.

Kwa upande wa Kilimanjaro, imeatoa vifaa mbalimbali vya elimu kwenye Shule za Sekondari wilayani Moshi vyenye thamani ya Sh.40 milioni ambapo Mkuu wa wilaya ya Moshi, Said Mtanda akipokea madawati na vifaa vya kuezekea alisema mchango wa wataendelea kuuenzi kwasababu unasaidia kupunguza changamoto za sekta ya elimu.

Shule zilizonufaika na vifaa hivyo ni Shule ya Msingi Mawalla, Shule ya Sekondari Mwika, Shule ya Sekondari Mangoto, Shule ya Sekondari Mieresini na Shule ya Sekondari Himo Sekondari zilizochangiwa mabati 293 na madawati 300 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya masomo kwa wanafunzi.

Mkoani Arusha, benki hiyo imetoa vifaa mabati, madawati, vitanda, viti na meza wa shule mbalimbali kutoka Wilaya za Arusha mjini, Arusha Vijijini, Karatu Meru Vijijini pamoja na Monduli Vijijini vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 45.

Katika Mkoa wa Simiyu wametoa madawati, meza na viti, mabati pamoja na mbao kwa ajili ya shule nne za msingi na Sekondari katika Wilaya ya Maswa vyote vikiwa na thamani ya Sh.24 milioni.

Akikabidhi vifaa hivyo, Meneja Kanda ya Magharibi Sospeter Magesse alisema NMB imetoa vifaa hivyo ili kuhakikisha mazingira ya wanafunzi kusomea yanakuwa mazuri ili watoto waweze kufikia malengo yao.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Aswege Kaminyoge akipokea vifaa hivyo ameishukuru benki hiyo, huku akiwataka walimu na wanafunzi kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa kwa makini ili kuweza kukaa muda mrefu.

Katika Mkoa wa Iringa, imetoa madawati 50 kwa shule ya msingi Itunduru yenye thamani ya Sh.5 milioni huku mkoani Rukwa katika shule ya msingi Mfaranyaki ikitoa mabati 200 yenye thamani ya Sh.6.25 milioni huku Hospitali mpya ya halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ikipatiwa vifaa vyenye thamani ya Sh.10 milioni.

Vifaa hivyo ni vitanda viwili kwa ajili ya kujifungulia wajawazito, vitanda 10 vya kulaza wagonjwa, magodoro 10, pamoja na mashuka 100.

error: Content is protected !!