December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Samia awapa neno wanaohoji ziara zake nje, mikopo

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema haendi nje ya nchi kucheza, bali anakwenda kutafuta fursa za maendeleo ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumapili, tarehe 17 Oktoba 2021, akihutubia wananchi wa Jiji la Arusha, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Kiongozi huyo wa awamu ya sita wa Tanzania, ametoa kauli hiyo akizungumzia faida zilizotokana na ziara zake nje ya nchi, ikiwemo kuondoa vikwazo vilivyokuwepo kati ya Tanzania na nchi husika.

“Kwa hiyo nikizunguka hivi msiseme mama anazunguka tu, sitazunguka bila sababu. Nilishacheza vya kutosha kwenye nchi nyingi duniani, lakini sasa hivi kazi ni moja tu kuzunguka kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ametolea mfano ziara yake aliyoifanya nchini Kenya, akisema imesaidia kufungua fursa za kibiashara za Mkoa wa Arusha.

“Ziara nilizofanya nchi jirani madhumuni kuondosha vikwazo vilivyokuwepo, kunyoosha njia ili wafanyabiashara wetu waweze kuuza ndani na nje, tukiondosha vikwazo na Kenya naambiwa biashara imekuwa zaidi ya mara sita kuliko ilivyokuwa wakati wa vikwazo,” amesema Rais Samia.

Wakati huo huo, Rais Samia amesema Serikali yake itaendelea kukopa mikopo nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Amesema hayo akizungumzia mkopo uliotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwa Serikali ya Tanzania, zaidi ya dola milioni 600 kwa ajili kukabiliana na athari za janga la Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19).

“Nataka niseme hii fedha tumekopa kwa masharti nafuu, kama leo umekosa kuchangishwa fedha za ujenzi wa madarasa, tunategemea utafanya kazi ulipe tozo, kodi na ushuru ili tukusanye kupata ya kurudisha,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Kaka yangu amesema tusiogope kukopa kama mikopo ndiyo hii, niwaahidi Watanzania nitaangalia mikopo yenye unafuu kwa nchi yetu, inayoleta faida kwa nchi yetu nitaichukua, mikopo chechefu sitoichukua. Lakini ile inayotusogeza sitaigopa nitaichukua.”

error: Content is protected !!