May 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Donald Trump ‘atua’ Mtambani

Spread the love

RAIS mpya wa Marekani, Donald Trump ametajwa kwenye Msikiti wa Mtambani, Kinondoni leo kama kiongozi aliyetangaza vita dhidi ya Uislam na Waislam, anaandika Mwandishi Wetu.

Kilichomsukuma Imam Suleiman wa Msikiti wa Mtambani, kumtaja Rais Trump, ni amri yake ya kuzuia raia wa nchi saba zinazochukuliwa kama zinazotii dini ya Kiislam, kuingia nchini humo.

Nchi hizo saba zilizokaliwa kooni na Trump, rais wa 45 aliyeapishwa Januari 20, mwaka huu, kumrithi Barrack Obama, ni Iran, Irak, Syria, Yemen, Libya, Somalia na Sudan.

Nchi hizi kwa mujibu wa amri ya rais Trump, raia zake wamepigwa mafuruku kuingia nchini Marekani kwa siku 90 kuanzia amri ilipotoka.

“Ni amri inayoonesha rais huyu mpya wa Marekani alivyo na chuki na Uislam na Waislam. Maana kama sababu ya amri yake ni tuhuma kuwa nchi hizo watu wake wanajihusisha na ugaidi, si kweli.

“Rekodi za mashirika ya kijasusi ya Marekani wenyewe zinaonesha kuwa tukio la ugaidi la 2001 lilihusisha raia 19 wa Saudia. Tukio jingine la 2015 la Carlifonia lilitendwa na raia wa Pakistan na tukio la 2016 ambalo wahusika wake hawajapatikana, lilisababishwa na mtu na mkewe ambao ni raia wa Pakistan.”

Amesema Imam Suleiman, “sasa kama watuhumiwa wakubwa wa matendo ya kigaidi ndani ya Marekani si katika raia wa hizi nchi saba anazozichukia, ni kwanini azuie raia zake kuingia Marekani?”

Ndipo hapo Imam Suleiman anaposema kwamba unapatikana ushahidi wa wazi kuwa Rais Trump anachukia Uislam na Waislam. “Tunapata nguvu kwa sababu hata kwa Waislam wanaoishi Marekani ambao wanatumia hati maalum iitwayo Green Card, wameanza kudhibitiwa kutokana na amri ya Trump.”

Imam Suleiman ambaye alieleza hayo katika khutba ya Ijumaa, ametahadharisha Waislam kuwa makini na kinachotengenezwa nchini Marekani kutokana na utawala mpya ulioshika madaraka.
Rais Trump katika amri yake hiyo, amesema halengi kudhibiti Waislam kwa kuwa ni sehemu muhimu ya raia wa taifa hilo.

error: Content is protected !!