May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

DK. SALIM AHMED SALIM; Mtanzania aliyemkaba koo George Bush

Spread the love

TAREHE 23 Januari, 2022 Waziri Mkuu Mstaafu Dk. Salim Ahmed Salim alitimiza miaka 80, leo nakuletea makala inayofafanua namna alivyombana pumzi aliyekuwa Rais wa 41 wa Marekani, George H.W Bush wakati huo Bush akiwa Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani, katika Umoja wa Mataifa.

Hii ilikuwa katika kikao cha 26 cha Mkutano uliofanyika mwaka 1971 huku ajenda kuu ikiwa ni ‘Urejeshaji wa Kisheria wa Haki za Jamhuri ya Watu wa China katika Umoja wa Mataifa. Hii ilikuwa ajenda namba 93.

Kikao hiki kilikuwa ni muendelezo wa vikao vilivyokaa kwa takribani miaka 22 kujadili nafasi ya uwakilishi halali wa China baina ya Jamhuri ya China (RoC) iliyokuwa chini ya Chiang Kai-Shek dhidi ya Jamhuri ya Watu wa China (PRC) iliyokuwa chini ya Mao Tsetung.

Kulikuwa na mgawanyiko mkubwa baina ya Marekani na Washirika wake ambao waliunga mkono uwepo wa uwakilishi wa Kai-Shek dhidi ya wale waliopinga uwakilishi huo na kutaka uwakilishi halali uwe wa Serikali ya Mao. Hawa waliongozwa na Albania.

Albania ikiongozwa na Mwakilishi wake wa Kudumu- Balozi Malile na washirika wake ilipeleka azimio lililotaka kutambuliwa kwa Jamhuri ya Watu wa China na Kufurushwa kwa Jamhuri ya China katika Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake Marekani ikiwakilishwa na George W. Bush ilipeleka Maazimio mawili wakitaka uwepo wa nchi mbili za China katika Umoja wa Mataifa yaani Taiwan ya Kai-Shek na China ya Mao.

Mao Tse – Tsung

Kwa upande mwingine Tunisia nao waliwasilisha maazimio matatu ambayo yalikuwa yanafanana kwa kiasi fulani na maazimio ya Marekani.

Kama hilo halitoshi Saudi Arabia nao waliwasilisha Azimio Namba A/L.638.

Maazimio ya Marekani, Tunisia na Saudi Arabia yalipelekwa kimkakati kwa lengo la kuvunja mpango wa Azimio la Albania na Washirika wake ikiwemo Tanzania ili usifanikiwe.

Kulikuwa na mtifuano mkubwa kuzuia Azimio la Albania lakini hatimaye lilikubaliwa kuwa ndiyo Azimio litakalopigiwa kura.

Ifahamike kuwa sababu kuu ya kupeleka maazimio hayo ilikuwa ni kutaka kusifanyike upigwaji wa kura wa Azimio namba A/L. 630 na nyongeza zake 1 na 2 siku hiyo ya tarehe 25 Oktoba, 1971 na badala yake upigwaji kura ufanyike kesho yake tarehe 26 Oktoba, 1971 ili Marekani na washirika wake wajipange kuzuia Azimio hilo kupitia maazimio yao waliyoyawasilisha mezani.

Kutokana na hali ilivyokuwa Dk. Salim Ahmed Salim alipewa majukumu mawili mahsusi, mosi kuzishawishi nchi za Afrika akiwa kama mhimili wa Kundi la Afrika katika Umoja wa Mataifa (African Group in the UN).

Mbali na kuzishawishi nchi za Afrika Dk. Salim alipewa pia jukumu la kuzishawishi nchi za Asia na Latini Amerika.

 

Kai – Shek

Pili, Dk. Salim alipewa jukumu la kuingilia kati jambo lolote lisilofahamika ambalo lilihitaji kuingiliwa kisheria kwa mujibu wa Kanuni za Mwenendo za Vikao vya Baraza la Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kuvunja kabisa mwendelezo wa jambo hilo kutoka upande wa upinzani.

Albania na washirika wake waliamini katika weledi na umahiri wa Dk. Salim katika kuzuia aina zozote za mbinu chafu kutoka kwa Marekani na washirika wake.

Haya yalikuja kutokana na ukweli kwamba kulikuwa na habari zilianza kusambaa ndani ya viunga vya Umoja wa Mataifa kuwa Rais Nixon wa Marekani alikuwa akielekea Peking kujadiliana namna ya kuifanya Taiwan ibaki ndani ya Umoja wa Mataifa.

Hivyo mpango wa Marekani ilikuwa ni kuipa nafasi China ya Mao sambamba na ile ya Kai-Shek yaani Taiwan.

Lengo la Marekani lilikuwa kuitumia Taiwan kuikwamisha China ndani ya Umoja wa Mataifa, jambo hili Albania, Tanzania na washirika wengine walilitambua na hivyo Dk. Salim alikuwa mtu rasmi aliyeteuliwa kufanya uingiliaji wa kimkakati kuvunja mpango huo wa Marekani.

Aidha, mpango wa Marekani na Washirika wake ilikuwa ni kuchelewesha upigaji kura mpaka pale Rais Nixon atakapotoka China na hatimaye kufanikiwa mpango wao huo wa kuigawa China (kuwa China Beijing na Taiwan).

 

Baada ya kubaini mpango huo, Albania, Tanzania na washirika wengine walishawishi Azimio hilo lijadiliwe tarehe 25 Oktoba, 1971 badala ya tarehe ambayo inaelezwa huenda ingesubiri Rais Nixon awe amerejea kutoka Peking hivyo kuathiri mchakato huo.

Baada ya kugundua mtego huo waliotegewa nao Marekani wakashawishi Azimio la Albania lijadiliwe kuanzia saa 4 asubuhi ili walau wajipange lakini kwa bahati mbaya kwao waliwahiwa na upande wa Albania na hivyo mjadala wa China kuanza saa 3 asubuhi, hili lilikuwa pigo lingine kwa Marekani.

Mtaalamu aliyekuwa akichezesha karata hizi na kumvuruga George H.W Bush na washirika wake alikuwa si mwingine bali ni Dk. Salim.

Baada ya kuona amekabwa koo hapumui, George H.W Bush aliomba kipengele chenye neno kufukuzwa kwa Kai-Shek kiondolewe.

George H.W Bush alitumia mbinu ya kujifanya anakubali Azimio la Albania na kusema kuwa wataliunga mkono Azimio A/L. 630 na nyongeza zake ikiwa kipengele chenye neno kufukuzwa kwa uwakilishi wa Chiang Kai-Shek kitaondolewa katika Azimio hilo.

Mtego huu wa Marekani ilikuwa ni kuwaingiza ‘kingi’ Albania, Tanzania na washirika wake ili hatimaye Taiwan iweze kubaki Umoja wa Mataifa kama nchi huru huku China nayo ikiendelea kuwepo kama Mwanachama wa Kudumu wa Umoja huo.

Dk. Salim alibaini ujanja huo wa George H.W Bush na Marekani yake na hivyo aliomba nafasi kujibu hoja, alipopewa nafasi akaendelea kumbana George H.W Bush kwa kuiainisha Kanuni ya 90 ya Kanuni za Mwenendo za Vikao vya Baraza la Umoja wa Mataifa kwa kuisoma.

Dk. Salim alimbainishia George H.W Bush kuwa upigaji wa kura ulikuwa tayari, hivyo haiwezekani kufanyia marekebisho Azimio ambalo tayari lipo kwenye kupigiwa kura.

 

Na kwa kukazia Dk. Salim akamsomea Kanuni ya 90 ya Kanuni za Mwenendo kwamba;

‘Mara tu Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa atakapotangaza upigaji wa Kura, hakuna mwakilishi, akiwemo wa Marekani (Hapa alimpiga dongo vijana wanasema) atakayeingilia upigaji kura isipokuwa kama kuna jambo la kanuni linalohusiana na upigaji kura.’

Kwa kusisitiza Rais wa Baraza hilo kwa wakati huo Adam Malik kutoka Indonesia nae akasema:

mapendekezo ya mabadiliko yaliyotolewa na Marekani hayawezi kupokelewa.

Baada ya kuona hivyo George H.W Bush wa Marekani na washirika wake walijiona kuwa wanaelekea kushindwa katika mkakati wao huo hivyo George H.W Bush alitoa pendekezo kuwa ili Azimio lionekane kuwa limepita ni lazima lipate theluthi mbili ya kura zote.

George H.W Bush alitoa pendekezo hilo akiamini kuwa Azimio hilo la Albania lisingeweza kufika theluthi mbili lakini kwa bahati mbaya alisahau kuwa Dk. Salim tayari alishapita kwenye kila kona kushawishi wajumbe wa Afrika, Asia na Latini Amerika.

Hatimaye Ajenda Namba 93 kuhusiana na ‘Urejeshaji wa Kisheria wa Haki za Jamhuri ya Watu wa China katika Umoja wa Mataifa ikapigiwa kura kwa kuzingatia Azimio lililowekwa mezani na Albania.

Azimio hilo lilielekeza kuirejeshea China ya Mao Tse-Tung kiti chake Umoja wa Mataifa na kuifurumusha China (Taiwan) ya Kai-Shek.

Azimio hilo lilipita kwa kura 76 za ndiyo huku 35 zikilikataa na 17 zikikaa kimya na nchi tatu hazikupiga.

Huyo ndiye Dk. Salim Mtanzania aliyemkaba koo George H.W Bush mpaka akashindwa kupumua ndani ya Baraza la Umoja wa Mataifa mwaka 1971.

Mwandishi wa makala haya ni Abbas Mwalimu – Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia anapatikana kwa simu namba +255 719 258 484

error: Content is protected !!