Monday , 6 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Dk. Biteko: Matumizi nishati safi ya kupikia yameanza rasmi
Habari Mchanganyiko

Dk. Biteko: Matumizi nishati safi ya kupikia yameanza rasmi

Spread the love

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amesema safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza rasmi nchini ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa  Serikali wa kuhakikisha kuwa wananchi na hasa kina mama wanahama kutoka matumizi ya nishati ya kupikia isiyo safi kwenda kwenye nishati iliyo safi na salama. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Amesema hayo leo tarehe 7 Machi, 2024 wilayani Temeke Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa hafla ya ugawaji mitungi ya gesi na majiko banifu ya kampuni ya ORYX Tanzania kwa wajasiriamali katika Soko la Temeke Stereo na Mbagala- Zakhem.

“Tunafahamu kwamba mwanamke ni mwathirika mkubwa nishati isiyo safi ya kupikia na wanapata madhara mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa kifua, kubakwa na kutumia muda mrefu kutafuta kuni, hivyo Serikali imeona kuwa ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi ili kumwezesha mwanamke kupata nishati safi na kwa gharama nafuu,” amesema Dk. Biteko

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa ni kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia siyo tu kwa Tanzania bali Afrika nzima na ulimwenguni.

“Hii ilithibitika wakati akizindua Programu ya Nishati safi ya kupikia itakayosaidia Wanawake Barani Afrika (African Women Clean Cooking Support Programme (AWCCSP) katika Mkutano wa Cop 28 Dubai ambayo imeungwa mkono na wadau mbalimbali hivyo kama nchi lazima iwe na mpango maalum wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema.

Ameongeza kuwa, zoezi hilo la ugawaji wa mitungi ya gesi na majiko banifu halitaishia Dar es Salaam bali ni endelevu na litafanyika katika mikoa mbalimbali nchini ili wananchi katika maeneo yote wahamasike kutumia nishati safi ya kupikia.

Dk. Biteko ametoa wito kwa viongozi wote wakiwemo wa dini, Serikali, jadi na makundi mengine kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia huku akisisitiza kuwa ajenda hiyo isiwe ya Serikali peke yake.

Pia ameomba wadau zaidi wajitokeze kuungana na Serikali katika suala hilo kama ilivyo kwa kampuni ya Oryx ambayo imeonesha kwa vitendo kuwa inaiunga mkono Serikali kwenye nishati safi ya kupikia.

Aidha, amezitaka Taasisi kama vile shule, magereza na hospitali watumie gesi kwenye matumizi ya kupikia na kuanza kubadilisha mifumo ya matumizi ya kuni kwenda kwenye gesi ili kufanikisha ajenda ya Serikali ya Matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Dk. Biteko pia amesisitiza utunzaji wa mazingira na misitu ili kuweza kupata maji ya uhakika, umeme na masuala mengine yanayotokana na utunzaji wa mazingira  na kueleza kuwa ili vizazi vijavyo visiishi kwenye jangwa  ni lazima kuchukua hatua sasa za kuzuia uharibifu wa mazingira.

Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema kuwa, hali ya upatikanaji umeme nchini ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam inaendelea kuimarika na kwamba kwa Mkoa wa Dar es Salaam kuna changamoto ya miundombinu ya kusafrisha umeme.

Hata hivyo, Serikali inatenga fedha za kuimarisha miundombinu hiyo ambapo laini ya umeme kutoka Gongolamboto kwenda Mbagala inaimarishwa kwa kujenga laini kubwa zaidi ya umeme na pia transfoma iliyopo Mbagala yenye ukubwa wa MVA 50 inabadilishwa na kuwekwa ya MVA 120.

Amesema pia inajengwa laini ya umeme chini ya ardhi ya kilometa 6 kutoka Kurasini kwenda Ilala ambayo itapunguza mzigo wa laini ya Mbagala na hivyo kufanya upatikanaji umeme kuwa tulivu na himilivu.

Kwa upande wake, Katibu wa Mama Lishe, Soko la Temeke Stereo, Mwanahamisi Nditi ameshukuru Serikali kwa kupata mitungi ya gesi na majiko banifu ambayo itawawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi kwenye soko hilo.

Ameeleza kuwa matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa na changamoto kwao kutokana na kufanya kazi kwenye moshi mwingi ambao unaathiri afya zao.

Pia ameomba kuwa zoezi hilo liendelee kutokana na uwingi wa mama lishe katika soko hilo ambao ni takriban 78  na wasaidizi wao wapatao 70.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali kutafuta mwekezaji mwingine Bandari ya Dar es Salaam

Spread the loveSERIKALI inaendelea kutafuta mwekezaji mwingine atakayeendesha gati namba nane hadi...

Habari Mchanganyiko

Tanzania  yasisitiza kuwa Kituo Kikuu cha Uchimbaji Madini Afrika

Spread the loveTanzania imeendelea kusisitiza adhma yake ya kuwa kituo kikuu cha...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga Hidaya chatikisa Mafia

Spread the loveWAKATI hali ya upepo mkali ikiendelea kushuhudiwa katika baadhi ya...

Habari MchanganyikoTangulizi

Usafiri baharini wasitishwa kukwepa athari za kimbunga Hidaya

Spread the loveUSAFIRI wa baharini umesimamishwa kwa muda ili kukwepa athari za...

error: Content is protected !!