OFISI ya Bunge la Tanzania imesema, wabunge kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na viongozi wa kisiasa nchini humo, wanakatwa kodi zote stahiki kwa mujibu wa sheria. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Miongoni mwa kodi hizo ni kodi ya mapato (PAYE), inayokatwa kwenye mishahara ya wabunge ya kila mwezi.
Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano na Uhisiano wa Kimataifa ya Bunge la Tanzania, iliyotolewa leo Jumanne, tarehe 3 Agosti 2021, imesema kinachoendelea kitandaoni kwamba wabunge hawalipi kodi kwenye mishahara hao hakina ukweli.
Ofisi hiyo ya Bunge, imetoa ufafanuzi huo baada ya siku za hivi karibuni, kuibuka taarifa mitandaoni kwamba, wabunge hawalipi kodi hivyo maumivu wanayoyapata kupitia tozo za miamala ya simu hawahusiki nayo.
Tozo hizo, zilianza kutumika tarehe 15 Julai 2021, baada ya kupitishwa na Bunge. Tozo hizo zimekuwa zikilalamikiwa na wananchi kwamba zinawaumiza na tayari Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameagiza zipitiwe upya kuangalia kama zinaweza kupunguzwa.
Leave a comment