Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa ACT: Hatutaacha kuikosa Serikali
Habari za SiasaTangulizi

ACT: Hatutaacha kuikosa Serikali

Dorothy Semu
Spread the love

WAZIRI Mkuu Kivuli kutoka ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amesema viongozi na wanachama wa chama hicho, hawataacha kuikosoa na kuishauri Serikali kwa kuhofia kukosa nafasi zinazohitaji kura kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Semu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo amesema hayo katika mahojiano, alipotembelea ofisi za gazeti la Raia Mwema na MwanaHalisi Digital Dar es Salaam.

Ameweka bayana kuwa hawako tayari kufungwa midomo, katika kukosoa na kushauri Serikali, kwa kuhofia kukosa jambo kutoka upande wa pili.

Amesema ACT-Wazalendo kupitia Kiongozi Mkuu wa chama walianzisha idara za wasemaji wa kisekta, baada ya kuona aina ya Bunge lililopo, haliruhusu kambi rasmi ya upinzani, hivyo wanachofanya ni kupigania na kusimamia maslahi ya umma.

Semu amesema kupitia wasemaji hao wa kisekta wamesaidia mambo mengi kama kuzungumzia malalamiko ya wananchi kuhusu tozo, kupanda kwa bei ya mafuta, ruzuku za mbolea kwa wakulima na mengine ambayo baadhi yamepatiwa ufumbuzi kwa kiwango fulani.

“Mimi hapa nimekuja kwenu kama Waziri Mkuu Kivuli, lakini pia wapo wasemaji wa sekta nyingine, msingi wa uwepo wa mfumo huu umejikita katika kusaidia, kukosoa na kushauri Serikali inapokosea, Bunge letu la sasa haliwezi kufanya haya.

“Sisi tumeanzisha huu utaratibu, wananchi wameupokea kwa mtazamo chanya, haturudi nyuma, tunachofanya ni kuendelea kuuboresha hasa kwa kutafuta vitendea kazi vya kisasa, lakini pia tunakaribisha vyama vingine makini kuungana nasi kusaidia nchi,” amesema Semu.

Amesema wanachosimamia wao ni hoja zinazogusa maisha ya Watanzania na si kuangalia maslahi binafsi, hivyo hawatakaa kimya kwa jambo linalopaswa kuzungumzwa au kukemewa.

Akijibu swali kuwa ukosoaji wanaofanya unatajwa kuwa sababu ya Katibu Mkuu wao, Ado Shaibu kukosa ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), amesisitiza kuwa wao walipeleka mtu makini na sahihi na hawakutaka hisani kwake na hawatafanya hivyo kwa yeyote, ilhali ukosoaji wao umejikita kwenye kupigania maslahi ya nchi.

“Tumejitokeza kisekta tukazungumzia sakata la Loliondo, Ngorongoro, mafuta kupanda bei nini kifanyike, ruzuku kwa wakulima na mauaji nchini na mengine, hilo ni jukumu letu na hatutarajii kupata ruhusa ya mtu, taasisi au chama chochote, eti kwa kisingizio cha kupendelewa, hiyo haitatokea,” amesema.

Makamu Mwenyekiti huyo akijibu swali kuhusu uwezo wa idara hizo za kisekta kutafuta taarifa na kujiendesha, amesema hiyo ni moja ya changamoto kubwa walizonazo, hivyo kuomba wadau kusaidia ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Dorothy amewataka Watanzania kutambua kuwa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), hakuwazuii kukosoa Serikali kwa kuwa sera na ilani inayotekelezwa ni ya CCM, hivyo yapo mambo ambayo wao hawakubaliani na njia sahihi ni kuzungumza mbele ya umma.

Amesema ushiriki wao katika Serikali hiyo hasa upande wa Zanzibar upo kikatiba na si suala la hisani, hivyo wataendelea kushiriki, kwa kuwa hawakufuata vyeo bali kushiriki kuchochea mabadiliko kwa jamii.

“Tuwekane sawa hapa, SUK si hisani au zawadi, ni jambo ambalo lililopo kikatiba, hivyo pale ambapo tunaona mambo hayako sawa hatuwezi kunyamaza lazima tuseme,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!