Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kina Mdee waanza kuhojiwa, Tendega aomba mahakama imlinde akitoa siri
Habari za SiasaTangulizi

Kina Mdee waanza kuhojiwa, Tendega aomba mahakama imlinde akitoa siri

Spread the love

 

MAWAKILI wa Chama cha Chadema, wameanza kuwahoji maswali ya dodoso wabunge  viti maalum nane kati ya 19, dhidi ya malalamiko waliyoweka katika hati zao za viapo, walizotumia kufungua kesi ya kupinga kufukuzwa ndani ya chama hicho. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wabunge hao wakiongozwa na Halima Mdee, walifungua kesi hiyo namba 36/2022, kuiomba Mahakama Kuu, Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam, kufanya mapitio ya kimahakama dhidi ya mchakato uliotumiwa na Chadema kuwafukuza, wakidai ulikuwa kinyume cha sheria kwani hawakupewa nafasi ya kusikilizwa na ulikuwa na mgongano wa kimaslahi.

Leo Kiongozi wa Jopo la Mawakili wa Chadema, Peter Kibatala, alianza kumhoji maswali ya dodoso Grace Tendega, mahakamani hapo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha. Maswali hayo yalitokana na malalamiko waliyowasilisha mahakamani hapo.

Mbali na Tendega, wabunge wengine ambao Mawakili wa Chadema wameomba kuwahoji ni Nusrat Hanje, EsterBulaya, Esther Matiko, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga na Cecilia Pareso.

Wakati Wakili Kibatala anaanza kumhoji maswali hayo Tendega, mwanasiasa huyo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA), aliiomba mahakama impe ulinzi endapo ataeleza mambo ambayo yatakuwa siri.

Wakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala (katikati) wakiwa mahakamani

Mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo:

Kibatala: Bila shaka mmefungua shauri hili namba 36/2022, mlisaini viapo mama na viapo vya kujazia?

Tendega: Nilisaini ndiyo.

Kibatala: Na Yale uliyosaini, uliyasaini baada ya kusoma na kuyaelewa?

Tendega: Nilisaini kwa uelewa

Kibatala: Unaweza kukumbuka tarehe 18 Julai ulikuwa wapi?

Tendega: Kabla ya kuendelea na mengine, nina swali

Jaji: Hapana, Leo hutauliza maswali. Leo utajibu maswali

Tendega: Nina swali, unavyoniona hapa nilikuwa kiongozi mkubwa katika Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA), nilikuwa katibu mkuu na nimeapa hapa nitasema kweli daima.

Naomba Jaji kwa sababu nimeapa nitasema kweli daima, unilinde nitakaposema mengine ambayo yatakuwa Siri.

Mimi ni kiongozi mkubwa naomba pia hilo nililinde

Jaji: Hutasema chochote ambalo sio jibu la swali unalosema, mawakili watauliza maswali utajibu watakayokuuliza. Ulinzi ni guarantee.

Jibu maswali ya Kibatala na baadae utajibu ya  Panya au wakili wako yoyote.

Baada ya Jaji Mkeha kutoa muongozo huo, Wakili Kibatala alieendelea kumuuliza maswali hayo ya dodoso kuhusu hati yake ya kiapo.

Akiendelea kumuuliza maswali ya dodoso Tendega, Wakili Kibatala aliiomba mahakama hiyo icheze video zilizokuwepo katika flash zilizowasilishwa mahakamani hapo na kina Mdee, kama vilelezo vyao vya ushahidi.

Ambazo zilikuwa na video zinazoonesha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, wakizungumza na wanahabari kuhusu sakata la kufukuzwa kwa wabunge hao.

Miongoni mwa hoja zao katika kesi hiyo, Mdee na wenzake wanadai adhabu iliyotolewa dhidi yao ilikuwa ni shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho, ambao katika nyakati tofauti walizungumza na wanahabari kuhusu sakata lao kabla ya vyombo husika kutoa maamuzi.

Video iliyoanza kuchezwa ilikuwa ya Mnyika, ambayo ilikuwa na takribani dakika tano, akitoa wito kwa Mdee na wenzake, kufika katika makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kujieleza dhidi ya tuhuma zilizokuwa zinawakabili.

Pia, katika video hiyo, Mnyika aliwaeleza wanachama wa Chadema kwamba chama hicho hakijateua majina ya wabunge viti maalum, huku akitoa wito kwa wafuasi hao kutoa maoni yao juu ya hatua za kuchukuliwa dhidi ya wanachama hao kufuatia msimamo wao kukubali kuapishwa kushika wadhifa huo, kinyume na msimamo wa chama.

Mhoajiano yao kuhusu video ya Mnyika yalikuwa kama ifuatavyo:

Kibatala:Unakubaliana kuwa Chadema kina wanachama nchi nzima?

Tendega: Ndiyo

Kibatala: Unafahamu kuwa nyie kula kiapo ilileta taharuki kwa wanachama?

Tendega: Sifaham

Kibatala: Kwenye Flash umesikia Mnyika akisema atapokea maoni ya watu?

Tendega: Nimesikia

Kibatala: Kwani walipeleka maoni yalipokelewa?

Tendega: Sijui

Kibatala: Kwani uamuzi ulikuw aunafanywa na watu au kamati kuu?

Tendega: Kamati Kuu

Kibatala: Maoni ya watu yalidhuru?

Tendega: Huyu alitoa kauli ni katibu mkuu wa chama, kwa nini asitumie wajumbe wa kamati kuu

Kibatala: Shahidi twende kwa kusikiliza hiyo klipu, kuna mahali anazungumza amesema kwamba nyie mtafukuzwa uanachama kama adhabu kwa hicho kilichotokea”

Tendega: Amesema tutawashughulikia

Kibatala: Mwisho kabisa kuhusiana na hiyo klipu, ni sahihi anasisitiza wewe na wenzako mhudhurie kikao cha Novemba 27, ili suala lenu kujadiliwa?

Tendega: Sikumbuki vizuri.

Baada ya Kibatala kumhoji maswali hayo Tendega kuhusu video ya Mnyika, wakili huyo aliiomba mahakama icheze flash iliyokuwa na video ya Mbowe, ambapo katika video hiyo, Mwenyekiti huyo wa Chadema anasema chama chake hakijawahi teua majina ya wabunge viti maalum.

Kutokana na video hiyo, Kibatala alimhoji Tendega kama ifuatavyo:

Kibatala: Kwenye kilelezo chako kuna maneno hujaweka?

Tendega: Ndio maana nimeweka dash dash ikimaanisha kuna maneno nimeyaacha

Miongoni mwa maswali ambayo Wakili Kibatala alimhoji Tendega, ni wapi aliposaini hati ya kiapo, ambapo mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:

Kibatala: Tarehe 18 Julai ulikuwa wapi? Tendega: Nilikuwa Dodoma

Kibatala: Angalia hati hii ya kiapo mwambie jaji kipao hicho ulichokiapa kama sehemu ya kuunga mkono maombi yako, ni cha kwako?

Tendega: Nakitambua hiki kiapo

Kibatala:Nakupeleka sehemu ambazo zinaonesha ukila kiapo ukiwa wapi, msomee jaji hapa kwenye tarehe kiapo kinasema ulisaini ukiwa wapi?

Tendega: Nikiwa Dar es Salaam

Kibatala: Tarehe 18 ulikuwa wapi?

Tendega: Mheshimiwa Jaji naomba nieleze zaidi hapo

Jaji:  Utajibu maswali ambayo unaulizwa, hayo maneno mawakili wako wataeleza ambapo hujaenda sawa sawa

Tendega: Nilithibitisha (hati ya kiapo) nikiwa Dar es Salaam, tarehe 18 Julai 2022.

Kibatala: Wakati huo ukiwa Dodoma si ndiyo?

Tendega: Kimyaa

Baada ya Wakili Kibatala kumaliza kumhoji Tendega maswali ya dodoso,m Jaji Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Alhamisi ijayo, tarehe 13 Oktoba 2022, ambapo ataulizwa maswali ya ufafanuzi na mawakili wao.

Pia, siku hiyo mawakili wa Chadema wanatarajia kuanza kumhoji mbunge mwingine viti maalum, Hawa Mwaifunga.

Mdee na wenzake wamefungua kesi hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!