RAIS wa Cameroon, Paul Biya amelaani ghasia zilizotekelezwa na wananchi na kusababisha mauaji ya watu nane wakati wa maandamano ya raia wa nchi hiyo, anaandika Catherine Kayombo.
Maandamano hayo yaliyofanywa na wazungumzaji wa lugha ya kingereza nchini humo wanaotaka kujitenga na kupewa eneo lao, yaliingiliwa kati na polisi na kusababisha raia hao kupigwa risasi.
Ghasia hizi zimetokea wakati wa maadhimisho ya miaka hamsini na sita tangu kujumuishwa kwa jimbo la wazungumzaji wa kiingereza ndani ya Cameroon.
Aidha rais Biya amewataka wananchi kutotenganishwa na itifaki za lugha kati yao, na kudai kuwa mgogoro wa lugha unaweza sababisha vita ya wao kwa wao.
Wazungumzaji wa lugha ya kingereza nchini Cameroon kwa uchache wao wamekuwa wakiandamana takribani mwaka sasa wakidai kubaguliwa hasa katika mfumo wa elimu na sheria ukilinganisha na wale wanaozungumza lugha ya Kifaransa.