VYOMBO vya habari nchini Uganda vimezuiwa kuonesha matangazo ya moja kwa moja (Mubashara) vikao vya Bunge vinavyoendelea nchini Uganda, anaandika Hamis Mguta.
Mkurugenzi wa Tume ya Utangazaji nchini humo, Godfrey Mutabazi amesema redio na televisheni zote haziruhusiwi kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja kuanzia leo Alhamisi.
Amesema Bunge limeamua kutoonyeshwa moja kwa moja kwa matangazo hayo kutokana na sababu za kiusalama.
Mapema leo, wabunge nchini humo wamepigana ndani ya ukumbi wa bunge wakiwa katika siku ya pili ya kikao cha kujadili muswada wa kuondoa ukomo wa miaka ya kugombea nafasi ya urais kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo.
Ugomvi huo ulianza pale Spika alipochukua hatua ya kuwafukuza wabunge wapatao 25 wengi wao wakiwa ni wale wa upinzani kwa madai ya utovu wa nidhamu pamoja na Waziri wa serikali aliyeshtakiwa kwa kufyatua risasi bungeni siku ya Jumanne.
Wabunge wa Chama tawala nchini humo wamefanikiwa kuwasilisha ombi la kuandaa mswada wa kubadilisha katiba na kuondoa kifungu kinachozuia mtu kuwania urais akiwa na umri wa zaidi ya miaka 75.
Leave a comment