Friday , 3 May 2024
Home Kitengo Biashara 2075 Waafrika kushika theluthi moja ya ajira
Biashara

2075 Waafrika kushika theluthi moja ya ajira

Spread the love

BENKI ya Dunia (WB), imesema ifikapo mwaka 2075, theluthi moja ya idadi ya watu watakaokuwa wanafanya kazi duniani watakuwa Waafrika. Anaripoti Selemani Msuya…(endelea).

Aidha, benki hiyo imesema kuanzia mwaka 2019 hadi 2022, imetoa dola bilioni 34 kwa ajili ya miradi ya maendeleo barani Afrika, huku dola bilioni 11.5 zikielekezwa kwa wanawake na wasichana.

Hayo yamesemwa jana tarehe 25 Julai 2023 na Mkurugenzi Mkazi wa WB nchini Tanzania, Nathan Belete wakati akifungua mkutano wa vijana uliondaliwa na Shirika la Save The Children ikiwa ni kuelekea Mkutano wa Viongozi wa Afrika kuhusu Rasilimali Watu wenye kauli mbiu ya ‘Kuongeza Kasi ya Ukuaji Kiuchumi Afrika, Kuimarisha Uzalishaji wa Vijana kwa Kuboresha Elimu na Ujuzi.’

“Hili ndio eneo pekee duniani ambapo nguvu kazi itaendelea kuongezeka katika miongo ijayo idadi ya watu wanaofanya kazi mwaka 2020 ilikuwa zaidi ya milioni 600, inatarajiwa kuongezeka watu milioni 450 ifikapo mwaka 2035 na mwaka 2075 itafikia bilioni 1.5,” alisema.

Alisema idadi hiyo ya watu milioni 450  na bilioni 1.5 ndizo takwimu ambazo zipo katika msingi wa majadiliano yao na katika mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika.

Mkurugenzi huyo alisema Afrika ni bara lenye nishati, ndoto, na uwezo mkubwa wa ukuaji wa kiuchumi haraka  ikiwa rasilimali watu wake zitatumika kwa usahihi.

“Rasilimali watu ni afya, maarifa na ujuzi ambao watu hukusanya katika maisha yao. Ndiyo inayobainisha uzalishaji na kipato cha mtu na mara nyingi ni mali pekee ambayo maskini wanayo.

Alisema dhana ya rasilimali watu inaanza kabla ya mtoto kuzaliwa na hukusanywa kwa kasi wakati wa utoto, ujana, na utu uzima, hivyo ili kuonesha matokeo chanya kunahitaji uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu tangu umri mdogo.

Belete alisema mwaka 2019, WB ilizindua Mpango wa Rasilimali Watu wa Afrika ambao umeweka malengo wazi na ahadi za kukuza uwezo wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kupitia rasilimali watu wake.

“Tangu wakati huo, nchi na jamii zimeongeza uwekezaji katika watu wa Afrika, ikiwa ni pamoja na kukuza wanawake na kuharakisha mabadiliko ya idadi ya watu Afrika.

Tuna nia ya kuimarisha malengo yetu ya kishujaa yaliyoainishwa katika mpango huo. Kati ya mwaka 2019 na 2022, ambapo ahadi za WB kwa shughuli za maendeleo ya binadamu barani Afrika zimefikia dola bilioni 34 na dola bilioni 11.5 zimeelekezwa kwa kuwawezesha wanawake na wasichana,” aliongeza.

Alisema fedha hizo zimeongeza kasi ya maendeleo katika uwekezaji na kwamba mkutano wa viongozi wa nchi kuhusu Rasilimali Watu wa Afrika utaongeza ahadi na kuweka vipaumbele kwa uwekezaji katika rasilimali watu kupitia ramani za nchi zinazounga mkono ujuzi wa kiufundi na fedha.

“Tunaamini kwamba tunapaswa kufanya zaidi na tunataka kushirikiana na ninyi vijana katika jukumu hili muhimu la kutia juhudi za haraka zinazohitajika kuwekeza katika watu wetu,” alisema.

Alisema WB inatambua vijana kama washirika katika juhudi hiyo ambayo wanaweza kusaidia kuzingatia suala la kipaumbele. “Ninyi ndio mustakabali na sauti yenu ni muhimu si leo tu katika tukio hili, bali pia katika kuendesha msukumo uliotokana na majadiliano haya,” alisema.

Belete alisema mkutano wa viongozi wakuu utaleta umakini na tahadhari katika ngazi ya juu kwa umuhimu wa kuwekeza katika watu kama msukumo mkuu wa uzalishaji, uthabiti na ukuaji.

Aidha alisema mkutano huo unaongeza uelewa wa fursa zinazowezekana kutokana na mabadiliko ya idadi ya watu katika eneo hilo kwa kuzingatia umuhimu wa kujifunza na ujuzi.

“Tunategemea mkutano utatoka na ahadi mbili hadi tatu za kifedha na sera zinazoweka uwekezaji katika watu kutoka kila nchi inayoshiriki na utaimarisha umiliki wa ajenda ya rasilimali watu na eneo hilo kama moja ya maeneo muhimu ya maendeleo endelevu chini ya Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika (AU),” alisema.

Alisema mkutano unalenga kuchochea ushirikiano zaidi wa kikanda na wa wafadhili kuhusu maendeleo endelevu ya rasilimali watu, haswa katika matokeo ya kujifunza na ujuzi.

Mkurugenzi huyo alisema majadiliano hayo hayapaswi kufikia kikomo leo, bali yanapaswa kuendelea kama hamasa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yang’ara maonesho OSHA

Spread the loveBenki ya NMB imebeba tuzo ya kampuni bora kwenye sekta...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC yashiriki maadhimisho Mei Mosi Arusha

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeungana na maelfu ya...

Biashara

Promosheni ya bil 1 kutoka Meridianbet kasino, cheza na ushinde zawadi kubwa

Spread the love  INGIA katika ulimwengu wa zawadi za kushangaza: Jishindie sehemu...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Equity Bank yaendelea kusotea mabilioni ya fedha mahakama rufani

Spread the loveBENKI za Equity ya Tanzania na Kenya, zimeendelea kupambana mahakamani...

error: Content is protected !!