Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini amesema kuwa, vitisho vya hivi karibuni vya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya nchi yake, ni vya kijinga, anaandika Hellen Sisya.
Kiongozi huyo amesema kuwa, vitisho hivyo ni kichekesho na ameonya kwamba, hadi sasa Marekani haijafahamu uwezo na nguvu kubwa ya Korea Kaskazini.
Amesisitiza kuwa , Pyongyang haiogopi Washington na kwamba, hata Maneva ya kijeshi ya Marekani yaliyofanyika hivi karibuni katika eneo la Korea na yale yanayoendelea sasa huko Australia, ni kujaribu tu kuonyesha uwezo wake uliozoeleka.
Eneo la Peninsula ya Korea limekuwa katika hali tete kutokana na siasa za uhasama zinazotekelezwa na Washington kwa kushirikiana na washirika wake kuilenga Korea Kaskazini. Kwa mara kadhaa Pyongyang imekuwa ikisisitiza kuwa, itaendelea kujiimarisha kijeshi madamu Washington itaendeleza vitisho vyake vya kila uchao dhidi yake katika eneo hilo.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, hadi sasa Marekani imefeli kwa kiasi kikubwa katika siasa zake za kupenda kujitanua kuihusu serikali ya Pyongyang na badala yake imebakia ikitumia shinikizo na vitisho pekee dhidi ya nchi hiyo.
Leave a comment