Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Zitto, Mwigulu Nchemba, waparurana
Habari Mchanganyiko

Zitto, Mwigulu Nchemba, waparurana

Spread the love

MBUNGE wa Iramba (CCM), Mwigulu Nchemba, amemvaa  mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Zuberi Kabwe, kwa kile alichokiita, “kukosa utu.” Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Kauli ya Mwigulu imekuja kufuatia Zitto, kukosoa hatua ya serikali ya Rais John Maguli, kuamua “kumwaga misaada” mbali mbali ya kibinadamu kwa mataifa ya Malawi, Zimbabwe na Msumbiji.

Akiandika kupitia ukurasa wake wa Twitter, Zitto anasema, siyo sahihi kwa serikali kutangaza misaada ya kibinadamu ya vyakula na madawa iliyotolewa na serikali kwa nchi za Msumbiji, Zimbabwe na ya Malawi.

Kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya habari, mataifa hayo matatu yamekubwa na kimbunga kikali cha Idai, kilichouwa maelfu ya watu na kuharibu mali kadhaa za wananchi na miundo mbinu ya serikali.

Kwa mujibu wa Zitto, hata mataifa mengine, yakiwamo mataifa yaliyojirani na Tanzania, hutoa misaada, “lakini kamwe haitumii nguvu kuitangazi kwenye vyombo vya habari.”

Zitto anasema, “hata wakati wa uongozi wa @jmkikwete (Rais Mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete), wenzetu wa Zimbabwe walipata maafa ya njaa. Serikali iliwapelekea chakula tani zaidi ya 8,000 za mahindi. Lakini hapakuwa na matangazo na tambo kama hizi za sasa.”

Anasema, “wala hapakuwa na tambo za kishamba shamba na kishetani namna hii. Unafanyia siasa msaada kwa wenzetu wenye maafa, tena bila hata aibu?”

Kiongozi huyo Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo anasema, “tulipopata tetemeko mkoani Kagera, majirani zetu kama Kenya na Uganda, walitoa misaada ya hali na mali na kamwe hawakujitamba kuwa #KenyaAid au #UgandAid.”

Lakini akijibu madai hayo ya Zitto, Mwigulu anasema, huwezi kutaka ustaarabu ambao wewe mwenyewe hauna; kila jambo linalofanywa na serikali mwanasiasa huyo wa upinzani amekuwa akiingiza siasa.

 “Kishamba Shamba na kishetani? Hii ni lugha ya mtu anayelilia ustaarabu pasipokuwa mstaarabu. Kwa utekelezaji mkubwa namna hii wa Ilani ya uchaguzi ya CCM (Chama Cha Mapinduzi), kwa jitihada za Rais.

“Hakuna kijiji hakijaguswa,…msaada ndio uwe wa kufanyia siasa? Usivyo na utu huoni utu, unaona siasa.”

Naye Zitto akijibu madai ya Mwigulu aliongeza, “hata Burundi walitusaidia. Nimeumizwa sana na tambo za watu wasio na utu kwa msaada tuliotangaza kuutoa Msumbiji. Hatuna Utu?”

Hii ni mara ya kwanza kwa Mwigulu kubishana kwenye mitandao ya kijamii, tangu alipotumbuliwa  na Rais Magufuli, Julai mwaka jana. Mwigulu alikuwa mmoja wa mawaziri wa kwanza katika serikali ya Magufuli.

Serikali ya Rais Magufuli kupitia kwa mawaziri wake wawili – Ummy Mwalimu, waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Prof. Palamagamba Kabudi, waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wamekabidhi msaada wa mamilioni ya shilingi kwa nchi za Malawi, Msumbiji na Zimbabwe, ili kusaidia kukabiliana na madhara ya kimbunga hicho.

Msaada huo, ulikabidhiwa jana tarehe 19 Machi 2019, kwa mabalozi wa nchi hizo waliopo nchini.

Misaada iliyokabidhiwa na serikali kwa mabalozi hao, ni pamoja na tani 200 za mahindi, tani 14 za mchele na tani 24 za madawa ya binadamu.

Zimbabwe, Malawi na Msumbiji, zimekumbwa na “kimbunga cha Idai” usiku wa Alhamisi ya tarehe 15 Machi 2019 na kuua watu zaidi ya 1,000 na kuharibu miundombinu huku wengine wakikosa makazi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

Habari Mchanganyiko

Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

Spread the loveNAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo...

Habari Mchanganyiko

Samia aagiza huduma za dharura maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya

Spread the love   RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia...

error: Content is protected !!