April 12, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli aifungulia Qatar milango ya uwekezaji

Rais John Magufuli

Spread the love

RAIS John Magufuli ameiomba nchi ya Qatar kushirikiana na serikali yake kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo uzalishaji wa nishati ya umeme na ujenzi wa miundombinu. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Rais Magufuli ametoa ombi hilo leo tarehe 21 Machi 2019 wakati akizungumza na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman J.A Al Than, Ikulu jijini Dar es Salaam.

 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, inaeleza kwamba mazungumzo hayo ya Rais Magufuli na Sheikh Mohammed yalijikita katika namna ya kuboresha uhusiano wa mataifa hayo mawili hasa kwenye sekta ya gesi na madini.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, Rais Magufuli alitangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini ikiwemo uchakataji wa gesi, madini, usafiri wa anga na utalii, na kumuomba Sheikh Mohammed kuwahamasisha wafanyabiashara wa Qatar kuja kuwekeza kwenye maeneo hayo.

“Natambua kuwa Qatar mna utaalamu wa kuchakata gesi na sisi tunayo gesi nyingi, kwa hivyo nawakaribisha mje tushirikiane kuwekeza katika sekta ya gesi na pia natambua kuwa nyie ni wanunuzi wakubwa wa dhahabu sisi tunayo dhahabu nyingi na hivi sasa tumeanzisha vituo vya ununuzi wa dhahabu. Nawakaribisha tutawapa ushirikiano wote mtaouhitaji,” amesema Rais Magufuli.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema baada ya Rais Magufuli na Sheikh Mohammed kuzungumza, atakunana na kiongozi huyo wa Qatar kwa ajili ya mazungumzo ya kina kuhusu maeneo ya ushirikiano.

Kwa upande wake Sheikh Mohammed, ameahidi kwamba Qatar itayafanyia kazi maombi ya Rais Magufuli ikiwemo kuzileta kampuni za nchi hiyo kuja kuwekeza katika maeneo yenye fursa zenye manufaa kwa pande zote mbili.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Fatma Rajab na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Abdullah Jassim Mohammed Al Medadi.

error: Content is protected !!