Friday , 29 September 2023
Home Kitengo Habari Kimataifa Wanajeshi Niger wadai kumpindua Rais
Kimataifa

Wanajeshi Niger wadai kumpindua Rais

Spread the love

KUNDI la wanajeshi wa Niger limetangaza kumuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum wa nchi hiyo, saa chache baada ya rais huyo kuzuiliwa ikulu na kikosi cha walinzi wa rais kinachoongozwa na Jenerali Omar Tchiani. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).

Taarifa iliyosomwa na Kanali Amadou Abdramane kupitia televisheni ya taifa jana Jumatano usiku, huku pembeni yake wakiwa wameketi wanajeshi wengine tisa, imeeleza kuwa vikosi vya ulinzi na usalama vimeamua kuuondoa utawala uliopo madarakani kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama, utawala mbovu na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Kanali Abdramane, mipaka ya nchi imefungwa na amri ya kutotoka nje imetangazwa nchi nzima na huduma katika taasisi zote za umma zimesitishwa, hadi hapo taarifa nyingine itakapotolewa.

 

Rais wa Niger, Mohamed Bazoum

Wanajeshi hao pia wameonya kuhusu uingiliaji wowote ule wa kigeni.

Hata hivyo, kundi la wanajeshi hao linalojiita Baraza la Kitaifa la Kulinda Nchi, limesema liko tayari kufanya mazungumzo na jumuia ya kitaifa na kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken ametoa wito wa kuachiwa mara moja kwa Rais Bazoum. Blinken amesema wanalaani matukio yanayoendelea Niger ya kunyakua madaraka kwa kutumia nguvu, ambayo yanaivuruga katiba ya nchi hiyo, pamoja na kudhoofisha utendaji kazi wa serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambaye ameonyesha uungaji wake mkono na Rais Bazoum, kwa kulaani matukio yanayoendelea Niger. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, amesema Guterres alizungumza kwa njia ya simu na Bazoum Jumatano jioni.

Guterres amelaani vikali juhudi za kunyakua madaraka kwa nguvu na kudhoofisha utawala wa kidemokrasia, amani na utulivu.

Amewataka wote wanaohusika kujizuia na kuhakikisha wanaheshimu na kuilinda katiba.

Rais Patrice Talon wa nchi jirani ya Benin, amesema yuko njiani kuelekea Niger kutathmini hali ilivyo, baada ya kukutana na Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS.

Aidha, Talon anatarajiwa kuwasili Niamey leo Alhamisi, ambapo atazungumza na pande zote mbili katika juhudi za kuutatua mzozo huo.

Umoja wa Afrika na ECOWAS wameliita tukio hilo kama jaribio la mapinduzi, na wamewataka waliopanga njama kumuachia huru Rais Bazoum bila masharti yoyote na warejee kwenye kambi zao.

Matukio yanayoendelea Niger yamelaaniwa pia na Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Benki ya Dunia ambazo zimesema kuwa zinafuatilia kwa karibu hali hiyo ambayo inaleta wasiwasi mkubwa.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais ya Niger usiku wa kuamkia leo, imeeleza kuwa Bazoum na familia yake wako salama, bila ya kutoa maelezo zaidi. Bazoum, mshirika wa karibu wa Ufaransa, alichaguliwa mwaka 2021 kuiongoza nchi hiyo isiyo na utulivu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Kimataifa

Wadukuzi wa Kichana waiba barua pepe 60,000 za Serikali ya Marekani

Spread the loveWADUKUZI wa kichana wamedukua barua pepe 60000 serikali ya Marekani...

Kimataifa

Mahakama yamkuta na hatia Donald Trump

Spread the love  ALIYEKUWA Rais wa Marekani, Donald Trump, amekutwa na hatia...

Kimataifa

Harusi yageuka msiba 100 wakifariki kwa ajali ya moto

Spread the love  WATU takribani 100, akiwemo bibi na bwana harusi, wamefariki...

Kimataifa

Kampuni ya mali ya China Oceanwide yapata agizo la kufilisiwa huko Bermuda

Spread the love  MAHAKAMA ya Bermuda imetoa amri ya kufilisiwa kwa Kamapuni...

error: Content is protected !!