Tuesday , 7 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wakongwe viti maalumu watakiwa kwenda majimboni
Habari za Siasa

Wakongwe viti maalumu watakiwa kwenda majimboni

Spread the love

JUKWAA la Wanawake Viongozi wa Jumuiya za Vyama vya Siasa nchini (ULINGO), limeshauri wanawake waliopata nafasi ya viti maalum zaidi ya mara moja, kuelekeza nguvu kwenye majimbo na kuachia vizazi vipya. Anaripoti Selemani Msuya…(endelea).

Aidha, vyama vya siasa nchini vimetakiwa kuweka kifungu kwenye Katiba zao kinacholazimisha uwakilishi wa watu wenye ulemavu na sio kuteuliwa kwa hisani.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Ulingo, Mama Anna Abdallah wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo jukwaa hilo lilikutana kwa siku moja kujadili miswada ya sheria mitatu iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, 2023.

Miswada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023.

Mama Anna alisema iwapo mwanasiasa mwanamke amepata nafasi ya kuwa mbunge wa viti maalum kwa awamu zaidi ya moja ni vema kuachia vijana wapya na yeye kushiriki kwenye majimbo, hali ambayo itawezesha jamii hasa vijana wa kike kutamani kushiriki siasa.

“Sisi tunaamini kugombea ni haki ya kila Mtanzania ambaye ana sifa za kugombea, na hivi viti maalum vilianzishwa ili kuwapa ujasiri wanawake katika siasa, hilo limefanikiwa sasa tuna asilimia 30 ya wabunge wa viti maalum, hivyo wanawake tuelekeze nguvu kwenye majimbo tukashindane na wanaume,” alisema.

Alisema Ulingo inatamani kuona wanawake wengi wanagombea kuanzia uenyekiti wa kitongoji, kijiji, mtaam, udiwani, ubunge na urais kwani ushahidi umeonesha kuwa wanaweza.

Mwenyekiti huyo alisema Rais Samia Suluhu Hassan ni ushahidi tosha kuwa wanawake wanaweza, hivyo ni jukumu la kila mmoja wapo kumsapoti mwanamke anaingia kwenye siasa.

“Sisi tunakauli yetu kuwa rafiki wa mwanamke ni mwanamke na jirani wa mwanaume ni mwanaume, tukienda na nguvu hii 2024 na 2025 tutafanya viziru sana, tupendane. Lakini tunaamini miaka 10 ya viti maalum inatosha, kwani hata upatikanaji wake kwa upande mwingine unatuzalilisha,” alisema.

Aidha, Mama Anna aliwaomba wapiga kura kutowachagua wabunge wa majimbo na viti maalum ambao hawatekelezi majukumu yao kwani ni kikwazo cha maendeleo.

Makamu Mwenyekiti wa Ulingo, Suzan Lyimo alisema suala la viti maalumu anaungana na wote wanaotaka ushiriki wa misimu miwili, ili kuwapa nafasi watu wapya.

“Nafasi ya viti maalum ni utaratibu wa kila nchi, ili kuwa na usawa, ila tunataka kuona mabadiliko baada ya kupata nafasi, lakini pia Katiba inatakiwa kusema wazi ni yapi majukumu ya mbunge wa viti maalum na hapa ndipo ajenda ya Katiba Mpya inaibuka,” alisema

Alisema wao kama wawakilishi wa wanawake nchini Tanzania wanasisitiza suala la jinsia katika nafasi mbalimbali ili dhana ya usawa iweze kutekelezeka.

Lyimo alisema pamoja na kupendekeza sheria hizo kuangalia eneo hilo la jinsia ni vema na Katiba za vyama vya siasa kuakisi ambacho wao wanakipigania kwenye Katiba mama.

“Sisi Ulingo tunajipanga kutoa hamasa kwa wanawake viongozi kuhamasisha wanawake wenzetu, ili washiriki uchaguzi kuanzia serikali za mitaa kwa wingi, kwa sababu tunaamini mwanamke akiongozi, anaongoza kama mama ndani ya familia, kwani anajua uchungu wa mtoto,” alisema.

Makamu Mwenyekiti huyo alisema siasa ni kila kitu, hivyo amewashauri wanaume kuondokana na dhana ya kuwa wanawake ni watu wa jikoni na hawawezi.

“Tuna Rais Samia mwanamke, Spika Dk Tulia Ackson mwanamke na tunaona wanafanya vizuri, hivyo tuwaunge mkono kwa sisi kushiriki chaguzi zote na tukipata nafasi ya kutoa maoni tutoe,” alisema.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Ulingo, Zanzibar Mgeni Hassan Juma alisema jukwaa hilo ni muhimu kwao kama wanasiasa wanawake kukutana na kuzungumza mambo yote ambayo yanawahusu.

Mgeni ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Wawakilishi alisema wao kama wanawake wanataka tafsiri ya Katiba inayosema haki sawa kwa wote iweze kuonekana katika utekelezaji na sio kuwepo kwenye maandishi pekee.

“Tumejipanga kuwasilisha maoni yetu bungeni, juu ya miswaada hiyo ambayo imewasilishwa bungeni, mfano inahitajika kuwepo uwiano wa asilimia fulani kuanzia ngazi ya chama na kwenye vyombo,” alisema.

Naibu Spika alisema uongozi wa Rais Samia umeonesha dunia kuwa wanawake wanaweza, hivyo ni dhahiri kwamba wakipewa nafasi katika uongozi wanaweza kusaidia nchi zao.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wanawake wenye Ulemavu Tanzania (SWAUTA), Stella Jailos alisema pamoja na mvutano wa uwepo wa viti maalum, bado kundi la watu wenye ulemavu halijapewa nguvu ya kisheria.

“Sisi watu wenye ulemavu hasa wanawake tunaomba vyama viweke vifungu kwenye Katiba zao ambavyo vitaelekeza kuwa ni lazima ikitokea viti maalum watu wenye ulemavu wawepo na sio hisani,” alisema.

Pia wanashauri mchakato wa kuwapata wanawake wenye ulemavu katika upande wa Zanzibar ukamilike hukohuko na sio kuwashindanisha na wa Tanzania Bara, huku akisisitiza kuwa iwapo mwakilishi huyo anafariki nafasi hiyo izibwe na kundi hilohilo.

Mkurugenzi huyo alisema kinachofanyika kuhusu viti maalum hakitafsiri dhana nzima ya maalum, hivyo ni nvema sheria zikabadilika na kuakisi hilo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Jacob, Malisa wapandishwa kizimbani kwa mashtaka ya uongo mitandaoni

Spread the loveMKURUGENZI wa Shirika la Haki, Godlisten Malisa na mwanachama wa...

BiasharaHabari za Siasa

Bunge laitaka Serikali kudhibiti ufisadi miradi ya mkakati

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka Serikali kuimarisha...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Wizara ya Uchukuzi yaomba kuongezewa bajeti na Bunge

Spread the loveWIZARA ya Uchukuzi imeliomba Bunge liidhinishe bajeti yake kwa mwaka...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali kutafuta mwekezaji mwingine Bandari ya Dar es Salaam

Spread the loveSERIKALI inaendelea kutafuta mwekezaji mwingine atakayeendesha gati namba nane hadi...

error: Content is protected !!