Wednesday , 8 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Waandishi waiburuta Quality Group ya Manji kortini
Habari Mchanganyiko

Waandishi waiburuta Quality Group ya Manji kortini

Spread the love

 

WAANDISHI wa habari nchini Tanzania waliokuwa waajiriwa katika Kampuni ya Quality Group Limited, wameiburuta kampuni hiyo mahakamani, wakishinikiza walipwe Sh.232 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Tangazo la kuitwa mahakamani kwa wawakilishi wa kampuni hiyo, lililotolewa jana Alhamisi na gazeti moja nchini, linawataka wawakilishi hao kufika mahakamani tarehe 20 Aprili 2022 saa tatu asubuhi, mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, E. M. Kassian.

“Mnapaswa kuhudhuria tarehe iliyopangwa bila kukosa na endapo hamtahudhuria ninyi au wawakilishi wenu wanaotambulika kisheria, maombi hayo yatasikilizwa bila uwepo wenu,” lilieleza tangazo hilo.

MwaanHALISI Online lilimtafuta mwakilishi wa waandishi hao 22 waliokuwa gazeti la JAMBO LEO, Joseph Lugendo, ambaye alikiri kuiburuta kampuni hiyo mahakamani, kudai fedha hizo zinazotokana na Tuzo ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Temeke, ya 24 Juni 2019.

Lugendo amesema tangu walipopata hukumu hiyo, wamekuwa wakiomba Kampuni hio itekeleze Tuzo hiyo, lakini haikuwahi kufanya hivyo.

Amesema walifikia uamuzi wa kuiburuta kampuni hiyo kortini kwa mara nyingine, ili kuomba Mahakama ikikubalika imkamate Mkurugenzi wake, Yusufu Manji, kwa kuwa ndiye aliyesaini barua za kusitisha ajira yao kinyume cha taratibu.

Amedai kabla ya tangazo hilo, waliiomba Mahakama itoe hati ya kumwita Manji na wawakilishi wa kampuni hiyo kortini, iliyotolewa 24 Februari 2022 lakini wanasheria waliokuwa wakiiwakilisha kampuni hiyo na Mkurugenzi huyo, walidai hawana mkataba tena na mteja wao huyo wa zamani.

Lugendo amesema baada ya kushindwa kumpata Manji, wala wawakilishi wa Kampuni hiyo, walirudi mahakamani 29 Machi 2022 kuomba kutangaza mwito huo gazetini, ili wawakilishi hao na/au Manji, wafike kortini kueleza sababu za kutolipa malipo hayo.

“Miongoni mwa waandishi ninaowawakilisha, wapo wanaodai Sh milioni 3 na hata wengine chini ya hapo. Kwa utajiri wa kampuni hiyo na Manji, hatuoni sababu za kushindwa kulipa madai yetu,” amesema Lugendo.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo ambayo MwanaHALISI Online lilipata nakala yake, hati ya kupinga kuondolewa kazini kwa waandishi hao iliwasilishwa kwa usuluhishi, ambao ulishindikana na baadaye 24 Oktoba 2017, ilihamishiwa kwa ajili ya uamuzi.

Ilidaiwa mbele ya Mwamuzi kwamba waandishi hao waliajiriwa katika kampuni hiyo katika nafasi mbalimbali kwa nyakati tofauti, lakini wote walisitishwa kazi siku moja ya 19 Septemba 2017.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, waandishi hao walidai kuajiriwa na Quality Group, lakini mikataba yao ilisitishwa kwa barua kutoka kampuni ya Quality Media Limited, na aliyesaini barua za kusitisha mikataba hiyo ni Manji mwenyewe.

Miongoni mwa waandishi hao, wapo waliodai mikataba yao ya ajira ilichukuliwa na mwajiri, hivyo walilazimika kuwasilisha barua ya kusitishwa kazi na hati ya kupokea mshahara kuthibisha kuajiriwa kwao.

Hukumu hiyo imeeleza kwamba kwa kuwa mlalamikiwa hakufuata utaratibu wa haki, katika kusitisha mikataba hiyo, waandishi hao wana haki ya kupewa sehemu ya mishahara iliyokuwa imebaki katika mkataba wao wa kazi, ambayo jumla yake ni Sh milioni 232.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

NBC, SILABU waungana kufikisha elimu ya fedha majumbani

Spread the loveBenki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya ushirikiano...

AfyaHabari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kisukari cha mimba ni nini?

Spread the loveKisukari cha mimba ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi...

Habari Mchanganyiko

Mafunzo kwa bodaboda 395 yamkuna Meya Dodoma

Spread the loveNAIBU Meya wa Jiji la Dodoma, Asma Karama amepongeza mafunzo...

Habari Mchanganyiko

Samia aagiza huduma za dharura maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya

Spread the love   RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia...

error: Content is protected !!