May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vifurushi: Kampuni za simu zapewa siku 30

Dk. Faustin Ndungulile

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imetoa mwezi mmoja kwa kampuni za mawasiliano ya simu za mkononi nchini humo, kuanza kutumia bei elekezi za vifurushi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Agizo hilo limetolewa leo Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile wakati akihojiwa na Kituo cha Runinga cha Clouds.

Akizungumzia agizo hilo, Dk. Ndugulile amesema, hadi kufikia tarehe 2 Aprili 2021, kampuni hizo zinapaswa kubadili mifumo yao ya vifurushi, ili iendane na bei elekezi ya serikali.

“Hadi kufikia tarehe 2 Aprili 2021, maagizo haya yote yawe yametekelezwa na wengine wameshaanza kutekeleza. Tumetoa mwezi mmoja sababu nao waende wakarekebishe kwenye mitambo yao,” amesema Dk. Ndugulile.

Akielezea mabadiliko hayo ya vifurushi vya simu, Dk. Ndugulile amesema, kwa mujibu wa bei elekezi mpya ya vifurushi vya data (internet), MB moja itauzwa kuanzia Sh. 2 hadi 9.

”Nimeingia ndani ya wizara hii tulikuwa hatuna bei elekezi ya mabando, hayakuwepo kama ilivyo katika umeme. Sasa hivi tumetoa bei elekezi ya data, itaanzia Sh. 2 hadi 9. Makampuni ya simu hayapaswi kwenda zaidi ya hapo kwa MB moja,” amesema Dk. Ndugulile.

Amesema, kampuni za simu hazitaruhusiwa kubadili aina za mabando, hadi zitakapopata ruhusa kutoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

“Bei elekezi tumeitoa, kampuni za simu yazingatie bei hizo. Hakuna upandishaji bei holela.”

“La pili, kuhakikisha hakuna holela tumeweka taratibu ambazo bando likizinduliwa leo na TCRA wakapitisha, hutaruhusiwa kufanya mabadiliko yoyote hadi miezi mitatu ipite unaweza ruhusiwa kubadili bando, hii italeta stability katika soko,” amesema Dk. Ndugulile.

Sambamba na bei elekezi hiyo, Dk. Ndugulile amesema mabadiliko hayo pia yatagusa muda wa vifurushi kuisha.

Katika mabadiliko hayo, kutakuwa na mabando yasiyokuwa na kikomo na wateja wataruhusiwa kugawa MB kwa watu ambao wako katika mtandao anaoutumia.

“La tatu wananchi walikuwa wanasema mabando yao yanaisha kabla ya muda, kutakuwa na bando lisilokuwa na ukomo utatumia mpaka liishe lakini wengine uwezo wao wa kununua bando bila ukomo,” amesema Dk. Ndugulile.

Dk. Ndugulile amesema “wako wenzangu hawana uwezo wa kununua bando la mwezi. Wananunua la siku au mwezi, mfano umenunua bando la mwezi una GB 10, umetumia umeona imebaki siku tatu na umebakiza GB tano.

“Kuna mambo mawili unaweza kufanya, sasa hivi una uwezo wa kuligawa kwa mwenzako wa mtandao ule ule. Au ukanunua GB nyingine kama una kifurushi kilichoisha muda, unanunua kingine zile GB tano zinaungana na hizo mpya,” amesema Dk. Ndugulile.

error: Content is protected !!