MAHAKAMA Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, imeahirisha usikilizwaji wa kesi iliyofunguliwa na wabunge viti maalum 19, kupinga kufukuzwa Chadema, kutokana na shahidi aliyetarajiwa kuendelea kuhojiwa na upande wa wajibu maombi, Hawa Mwaifunga, kuumwa mgongo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kesi hiyo Na. 36/2022, iliyotarajiwa kuendelea kusikilizwa leo Ijuma, tarehe 21 Oktoba 2022, imeahirishwa na mahakama mbele ya Jaji Cyprian Mkeha, baada ya Mwaifunga kupitia mawakili wake, kuomba ahirisho akidai anaumwa mgongo.
Mwaifunga kupitia mawakili wake, aliwasilisha madai ya kuugua, katika kikao cha majadiliano mafupi kati ya Jaji Mkeha na mawakili wa waleta maombi na wajibu maombi,ambapo Jaji Mkeha aliahirisha kesi hadi tarehe 3 Novemba mwaka huu.
Mawakili wanaomuwakilisha Mwaifunga na wenzake 18 katika kesi hiyo ni, Emmanuel Ukashu, Ipilinga Panga, Edson Kilatu na Aliko Mwamanenge.
Siku hiyo, Mwaifunga ataendelea kuulizwa maswali ya dodoso kuhusu malalamiko yake aliyoyaweka kwenye hati yake ya kiapo na hati ya kiapo cha pamoja na mawakili wa mjibu maombi wa kwanza, Bodi ya Wadhamini ya Chadema.
Mbunge huyo ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (BAWACHA), alianza kuhojiwa maswali hayo na Kiongozi wa Jopo la Mawakili wa Chadema, Peter Kibatala, tarehe 13 Oktoba 2022, baada ya mbunge mwenzake, Grace Tendega kumaliza kuhojiwa maswali hayo.
Aidha, Jaji Mkeha amepanga tarehe nyingine za kusikilizwa kesi hiyo kuwa ni 4,5,8,9 Novemba 2022 na tarehe 6, 7 Desemba mwaka huu.
Katika tarehe hizo, mawakili wa Chadema wataendelea kuwahoji wabunge sita waliobakia, kati ya nane waliyoruhusiwa na mahakama hiyo kuwahoji ili watoe ushahidi wao kuhusu hati zao za viapo.
Wabunge hao sita walioitwa kuhojiwa na Chadema ni, Ester Bulaya, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Esther Matiko, Cecilia Pareso na Halima Mdee.
Leave a comment