Friday , 3 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Waislamu wataka sheria mpya ya ndoa isiwatambue
Habari Mchanganyiko

Waislamu wataka sheria mpya ya ndoa isiwatambue

Sheikh Issa Ponda, Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu
Spread the love

JUMUIYA na Taasisi za Kiislamu Tanzania, imetoa msimamo wake kuhusu marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya 1971, ikitaka isiwatambue waumini wake kwa kuwa suala hilo ni la kidini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Msimamo huo umetolewa leo Ijumaa, tarehe 21 Oktoba 2022 na Katibu Mkuu wa Jumiya hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda, ametoa mapendekezo ya jumuiya hiyo, ikiwa imepita siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan, atoe wito kwa wadau kutoa mapendekezo yao kwa ajili ya kuboresha muswada wa maboresho ya Sheria ya Ndoa, uliotinga bungeni Septemba mwaka huu.

Taarifa ya Sheikh Ponda imeeleza kuwa, wasilamu wana sheria yao ya ndoa na kwamba hawana tatizo nayo, lakini pia muislamu asiyeitambua sheria hiyo ameruhusiwa  na katiba ya nchi kufunga ndoa ya Serikali au ya dini atakayohamia.

“Kwa mujibu wa katiba ya nchi, jukumu la sheria za ibada limeachwa katika vitabu vitakatifu vya dini, Quran na Sunna ya Mtume Muhammad (S.A.W). Msimamo wetu wetu suala la ndoa liachwe katika dini husika, Serikali itunge sheria ya ndoa kwa wasiokuwa na sheria hiyo, Serikali itunge sheria ya ndoa kwa dini itakayopeleka maombi,” imesema taarifa ya Sheikh Ponda.

Licha ya msimamo huo, jumuiya hiyo  imetoa mapendekezo yake kwa Serikali kuhusu marekebisho ya Sheria ya Ndoa yenye lengo la kuiboresha ili itoe uhuru kwa waumini wa kiislamu kutekeleza sheria na kanuni zilizoko katika Quran tukufu, hususan katika masuala ya ndoa, talaka na mirathi.

 “Kumekuwa na mivutano mikubwa kati ya Serikali na jamii ya waislamu katika masuala ya ndoa, talaka, malenzi ya watoto na mirathi kwa muda mrefu, mivutano hiyo imekuwa na athari mbaya hasa kwa waislamu na dini yao. Bado tunayo matumaini kwa Serikali kuzingatia uhuru na haki ya waislamu kufuata ndoa kama katiba ya nchi inavyoelekeza,” imesema taarifa ya Sheikh Ponda.

Kwa mujibu wa taarifa ya Sheikh Ponda, waislamu wanapendekeza umri wa msichana kuolewa au mvulana kuoa ubaki vilevile, kwa kuwa unaendana na sheria za dini ya Kislamu, zinazotaka mtu aoe akishabalehe au aolewe akishavunja ungo.

Sheria ya sasa ya ndoa, inaelekeza umri wa kuolewa ni miaka 14 kwa ruhusa ya mahakama, 15 kwa ridhaa ya wazazi na 18 na kuendelea kwa ridhaa ya anayeolewa.

“Miaka ya 1971 wakati Serikali ikitunga sheria yake ya ndoa inasemekana makisio ya balehe yalikuwa miaka 14 hadi 15 kwa msichana na mvulana miaka 18. Katika dini ya uislamu na sheria yake, umri wa kuoa au kuolewa unapatikana kwa mhuisika kufikia balehe. Waislamu hatutahusika na sheria inayokinzana na umri uliolekezwa na Quran tukufu,” imesema taarifa ya Sheikh Ponda.

Taarifa ya Sheikh Ponda imedai kuwa, pendekezo la Serikali kuongeza umri wa ndoa, itachochea vijana wanaobalehe kabla ya muda husika kukiuka maadili yao kwa kutafuta mbinu za kufanya vitendo vya ngono kisiri, ikiwemo usagaji na kinyume na maumbile (ushoga).

“Vijana hawa wanazuiliwa haki ya kimaumbile, watatafuta mbinu nyingine za kukidhi haja zao kwa siri na kinyume na maadili, njia hizo ni pamoja na usagaji na ushoga, baada ya kuingia huko hawataona faida ya ndoa bali wataendelea na matendo hayo machafu,” imesema taarifa ya Sheikh Ponda.

Pendekezo lingine lililotolewa na jumuiya hiyo, ni sheria mpya ya ndoa itambue talaka zinazotolewa kwa mujibu wa Quran na sunna, kama inavyotambua ndoa za kiislamu.

Taarifa ya Sheikh Ponda imesema kuwa, waislamu wanapendekeza sheria ya ndoa iweke bayana tafsiri ya ndoa za utotoni, kwani ya sasa hivi imeweka mwanya wa mtu kutambua ndoa ni ya utotoni au siyo ya utotoni kulingana na umri uliowekwa kwenye sheria hiyo. Wamependekeza, ndoa ya utotoni itambulike kuwa ni ile mhusika amefunga  kabla ya kubalehe.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga “HIDAYA” chaendelea kuimarika, wananchi wapewa tahadhari

Spread the loveMAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yang’ara maonesho OSHA

Spread the loveBenki ya NMB imebeba tuzo ya kampuni bora kwenye sekta...

Habari MchanganyikoKimataifa

Ruto amteua Kahariri kuwa mkuu wa majeshi

Spread the loveRAIS wa Kenya, William Ruto, amemteua Jenerali Charles Muriu Kahariri,...

error: Content is protected !!