October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Uchaguzi mkuu Angola kuzika zama za chama kimoja?

Adabberto Costa Junior

Spread the love

WAPIGA  kura nchini Angola wanapiga kura leo tarehe 24 Agosti, 2022 kumchagua rais mpya. Uchaguzi huo umetajwa kuwa na ushindani mkali kuwahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa siasa za vyama vingi nchini humo mwaka 1992.

Chama cha Peoples Movement for the Liberation of Angola – MPLA, kimetawala Angola tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1975.

Chama kikuu cha upinzani cha The National Union for the Total Independence of Angola (UNITA), kimepata umaarufu mkubwa nchini humo kinyume na ilivyokuwa katika uchaguzi wa awali.

Angola ambayo ni mzalishaji mkubwa wa pili wa mafuta Barani Afrika, ilikumbana na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa muda wa miaka 27.

Rais Joao Lourenco (kulia) akiwa na Rais wa zamani wa taifa hilo Jose Eduardo dos Santos enzi za uhai wake.

Tayari Chama cha upinzani cha UNITA kimeishutumu serikali kwa kujaribu kulazimisha utawala wa chama kimoja na kwamba kinafikiria kupinga matokeo ya uchaguzi ambao chama hicho kinaona kwamba huenda usiendeshwe kwa njia ya haki.

Kiongozi wa chama hicho Adabberto Costa Junior amesema kwamba utawala wa MPLA, hautaki kabisa Angola kuwa nchi yenye demokrasia.

UCHAGUZI UTATAWALIWA NA UWAZI?

Baadhi ya wakosoaji wa serikali wameelezea wasiwasi kwamba huenda uchaguzi ukashindwa kumpata mgombea aliyechaguliwa na wapiga kura, maana yake kwamba huenda ukajaa wizi wa kura.

Kuna waangalizi 2,000 pekee wanaofuatilia uchaguzi wa Angola, nchi ambayo ni kubwa mara mbili ya Ufaransa.

Hesabu ya mwisho ya kura itatangazwa mjini Luanda na baadhi ya vituo vya kupigia kura vimewekewa masharti ya kutotangaza matokeo hayo.

Chama kinachotawala cha MPLA, kimekataa maombi ya vyombo vya habari kujibu shutuma hizo na hakijatoa taarifa yoyote, lakini kilisema awali kwamba kitakubali matokeo ya uchaguzi huo.

UDHIBITI WA SERIKALI KWA TAASISI ZA UMMA

Wanasiasa wa upinzani na mashirika ya kiraia yameishutumu serikali ya MPLA kwa kudhibiti taasisi za serikali ikiwemo mahakama na vyombo vya habari.

Rais wa Angola anayeteta ungwe yake ya pili, Joao Lourenco, naye hajazungumzia shutuma hizo lakini aliwahi kusema mwanzoni mwa mwaka huu kwamba mahakama za Angola zina uhuru wa kufanya kazi yake bila ya kuingiliwa.

Lourenco aliteuliwa na Jose Eduardo dos Santos, aliyeachia madaraka mwaka 2017, baada ya kutawala nchi hiyo kwa muda wa miaka 38.

Lourenco anagombea muhula wa pili huku upinzani ukiwa umetishia kupinga matokeo.

Aidha, Lourenco ameahidi kupambana na ufisadi, kuimarisha ukuaji wa uchumi na kuimarisha demokrasia.

Lakini Costa Junior amesema kwamba ahadi anazotoa rais wa sasa hazijawahi kutekelezwa na utawala wake na kwamba hakuna mabadiliko yanayoonekana kutekelezwa ili kuimarisha hali ya maisha kwa watu wa Angola.

 

Costa amesema kwamba iwapo matokeo ya uchaguzi hayatakuwa huru na haki, watatumia njia zote za kitaifa na kimataifa, wanazoweza kuzitumia, kupinga matokeo hayo.

Amesema kwamba chama chake tayari kina ushahidi kwamba kanuni kadhaa za uchaguzi zimekiukwa lakini ana imani kwamba tume ya uchaguzi itatekeleza mabadiliko kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Pamoja na madai hayo, Chama cha MPLA kimekataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu madai ya upinzani.

Costa Junior amewataka wapiga kura kubakia kwenye vituo vya kupiga kura baada ya kupiga kura yao ili kuhakikisha kwamba hakuna udanganyifu unafanyika.

MWILI WA JOSE EDUARDO DOS SANTOS WAWASILI LUANDA

Wakati wapiga kura wakitekeleza haki yao ya kikatiba, mwili wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Jose Eduardo dos Santos umerudishwa nchini humo.

Dos Santos alifariki akipatiwa matibabu nchini Spain, mjini Barcelona, mwezi Julai mwaka huu.

Mwili wa Eduardo dos Santos umewasili Luanda, baada ya kusubiriwa kwa muda mrefu.

Wachambuzi wamesema hatua ya mwili wa Santos kurudishwa nchini wakati wa uchaguzi ni ya kisiasa.

Mwili wa Santos umerudishwa Angola baada ya kutokea hali ya kutoelewana  kati ya familia yake na serikali kwamba kuhusu madai kwamba aliuawa.

Santos alifariki Julai 8 mwaka huu, akiwa na umri wa miaka 79 akitibiwa mjini Barecelona ambako alikuwa amelazwa kwa muda mrefu.

Kesi kuhusu kifo chake ilifikishwa mahakamani na binti yake Tchize dos Santos akidai kwamba huenda rais huyo wa zamani aliuawa. Baada ya uchunguzi wa kina kwa mwili wake, mahakama  ilisema kwamba alikufa kifo cha kawaida baada ya kuugua.

Familia yake ilikuwa imetaka mwili wake kuzikwa Barcelona, lakini mahakama ikaamua kwamba urudishwe Angola.

Rais Lourenco, ametoa wito kwa wapiga kura kupigia kura chama kinachotawala, kama heshima kwa hayati Dos Santos.

Hatua hiyo inatafsiriwa na wachambuzi, mazishi yake yatatumika kwa manufaa ya kisiasa.

Itakumbukwa kuwa licha ya Rais wa sasa kuteuliwa na Dos Santos, aliagiza uchunguzi wa madai ya ufisadi wakati wa utawala wa Dos Santos uliohusisha mabilioni ya dola.

Marekani ilimuwekea vikwazo mwaka 2021, binti wa dos Santos kwa kuhusika katika kashfa ya mabilioni ya dola fedha za umma kwa manufaa yake binafsi.  Kashfa hiyo ilifichuliwa na waandishi wa habari wapelelezi mwaka 2020.

error: Content is protected !!