Tuesday , 7 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Tume huru ya uchaguzi kaa la moto
Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi kaa la moto

Spread the love

KITENDO cha Serikali kuanza kutumia sheria mpya ya tume huru ya taifa ya uchaguzi ya 2024, pasina kubadili muundo na utendaji wa tume, kimeendelea kupigwa vita na wanasiasa wa vyama vya upinzani na watetezi wa haki za binadamu Tanzania.Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Tangu Serikali itangaze kuwa kuanzia leo tarehe 12 Aprili 2024, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itatambulika kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mijadala imeibuka katika majukwaa mbalimbali huku asilimia kubwa ya washiriki wake wakipinga uamuzi huo wakidai ni batili.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Tundu Lissu, akizungumza na Kituo cha Redio cha Clouds, leo Ijumaa, amedai tume hiyo haitakuwa huru kwa kuwa wateule wake bado wanawajibika kwa Rais.

“Utaratibu bora wa kuhakikisha mtu hateui kwa maslahi yake ni huu ufuatao, Hiyo inayoitwa kamati ya usaili inatakiwa iwe huru na inakuaje huru? Inakuwa haiwajibiki na huyo inayomshauri, siyo watu wanaopewa kazi na huyo wanayemshauri, Kenya ni mfano mzuri sana, watu ambao wanaingia kwenye kamati ya usaili ni majaji, wajumbe wa tume huru ambazo zinaitwa tume au taasisi huru, halafu hiyo kamati ya usaili inaitisha maombi inafanya usaili inachuja na kupendekeza majina,” amesema Lissu.

Lissu amesema “baada ya hapo majina hayo yanapelekwa bungeni kujadiliwa, na yakishajadiliwa na bunge na kupitishwa anapelekewa Rais , Rais anapelekewa kutia baraka tu hawezi kusema ‘hawa siwataki’, anateua kwa jinsi ambavyo huo mchakato umefanywa, kwa hiyo tume huru ya mipaka na uchaguzi ya Kenya imeundwa kwa utaratibu huo, watu wanaomba kazi wanasailiwa na chombo huru, wanafanyiwa mchujo, wanapelekwa bungeni, wanapitishwa au kukataliwa na bunge baada ya hapo anapelekewa Rais anaambiwa ‘watu wetu ni hawa fanya uteuzi.’”

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Onesmo Olenguruwa, amesema ili tume hiyo iwe halali inabidi viongozi walioko madarakani wajiuzulu ili wateuliwe wapya kwa kuzingatia matakwa ya sheria mpya.

Matakwa ya sheria mpya kuhusu namna ya kuwapata viongozi wa INEC, ni wanaohitaji nafasi hizo kuomba uteuzi, kufanyiwa usaili na kisha majina yao kuchujwa na kamati ya usaili itakayoundwa ambayo itawailisha majina ya watu waliokidhi vigezo kwa Rais kwa ajili ya uteuzi.

“Ili sheria iweze kufanya kazi vizuri na malengo ya Rais Samia na watanzania kuwa na tume huru yatimie, lazima tume ya sasa ijiuzulu ili mfumo mpya wa tume uanze kwa kuzingatia matakwa ya sheria mpya. Hauwezi kuipata tume huru kwa kubadilisha jina tu ni lazima ubadilishe muundo bila ya hivyo tutakuwa tumekwama hatutakuwa na tume huru,” amesema Olengurumwa.

Olengurumwa amesema kwa sasa tume hiyo ni batili kwa kuwa kabla ya sheria hiyo kuanza kutumika ilipaswa katiba ifanyiwe marekebisho madogo ili kuipa nguvu.

“Mambo mengi ambayo yanatakiwa yafanyike kupitia sheria mpya ya tume huru ya uchaguzi, yangeanza kufanyiwa kazi kwenye katiba, mfano katiba ilipaswa ianze kuweka wazi kwamba chaguzi zote za rais na serikali za mitaa zitasimamiwa na tume, iweke wazi namna gani viongozi watapatikana na muundo wake,” amesema Olengurumwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Jacob, Malisa wapandishwa kizimbani kwa mashtaka ya uongo mitandaoni

Spread the loveMKURUGENZI wa Shirika la Haki, Godlisten Malisa na mwanachama wa...

BiasharaHabari za Siasa

Bunge laitaka Serikali kudhibiti ufisadi miradi ya mkakati

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka Serikali kuimarisha...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Wizara ya Uchukuzi yaomba kuongezewa bajeti na Bunge

Spread the loveWIZARA ya Uchukuzi imeliomba Bunge liidhinishe bajeti yake kwa mwaka...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali kutafuta mwekezaji mwingine Bandari ya Dar es Salaam

Spread the loveSERIKALI inaendelea kutafuta mwekezaji mwingine atakayeendesha gati namba nane hadi...

error: Content is protected !!