Friday , 29 September 2023
Home Kitengo Maisha Elimu TCU yatoa maelekezo tisa, yaonya vyuo
Elimu

TCU yatoa maelekezo tisa, yaonya vyuo

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa
Spread the love

TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imetoa maelekezo tisa yanayopaswa kufuatwa vyuo vya elimu ya juu na waombaji wapya katika mchakato wa udahili unaondelea kwa sasa. Anaripoti Selemani Msuya…(endelea).

Aidha TCU imesema haitasita kuchukua hatua kwa vyuo ambavyo vitakwamisha waombaji wa vyuo kushindwa kufanya udahili kwa vyuo wanavyotaka.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Prof Kihampa amezitaka taasisi za elimu ya juu kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika zoezi la udahili ili kuepusha usumbufu usiokuwa na lazima kwa waombaji wa udahili.

Prof Kihampa amewataka waombaji kusoma miongozo ya sifa ya kujiunga na program husika, ili kuona wanakidhi vigezo kabla ya kutuma maombi ya udahili.

Pili aliwataka waombaji wenye changamoto ya kupokea namba za siri ya uthibitishaji katika chuo kimoja, kuingia  kwenye mifumo ya udahili wa vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa namba maalum ya siri ili kuweza kuthibitisha katika chuo husika.

Alisema pia waombaji wanashauriwa kutumia barua pepe au mitandao ya simu na udahili ufanyike kupitia akaunti ambayo muombaji alitumia kuomba udahili mwanzoni.

“Taasisi zote za elimu ya juu zinazofanya udahili ziruhusu waombaji kuingia katika mifumo yao na kuwapa namba ya siri ili wafanya udahili na kuthibitisha wao wenyewe,” alisema.

Alisema pia taasisi za elimu ya juu zihakikishe waombaji udahili wanajithibitisha wao wenyewe kupitia akaunti zao na si vinginevyo na wanaotaka kubadili uthibitisho waingie katika akaunti za vyuo, ili wajithibitishe katika chuo kingine.

“Waomba wanaotaka kubadili maombi wafute maombi ya awali na kutuma mapya na vyuo vinatakiwa kutoa elimu kwa umma namna sahihi ya kuwasiliana na vyuo husika ili kuepuka udanganyifu unaoweza kujitokeza,” alisema.

Pia Prof Kihampa alisema zoezi la kutuma maombi ya udahili kwa wanafunzi waliopata chuo zaidi ya kimoja linaenda vizuri ambapo hadi jana jumla ya waombaji 23,387 wamethibitisha kati ya 43,213 wanaopaswa kufanya hivyo.

Kihampa aliwataka waombaji ambao hawajathibitisha wakamilishe uthibitisho wao kupitia akaunti zao kwenye vyuo wanavyopenda na kwamba hakuna mwanafunzi atakayekosa chuo kwa kushindwa kuthibitisha.

Akifafanua kuhusu taarifa za vyuo kushiriki kukwamisha waombaji kujidahili katika vyuo wanavyotaka Kihampa alisema TCU imejipanga kuhakikisha waombaji wote wanapata udahili bila kukwamishwa na mtu yoyote.

Kihampa alisema jukumu la vyuo ni kushirikiana na wanafunzi ambao wanataka kufanya udahili wa kujiunga na vyuo vyao na si vinginevyo.

“TCU tupo makini sana katika mchakato wa udahili ambao unatumia mifumo zaidi, hatutasita kuchukua hatua kwa chuo ambacho kitabainika kukwamisha wanafunzi kufanya udahili kwenye chuo anachokitaka,” alisema.

Katibu huyo alisema hakuna muombaji wa udahili ambaye atanyimwa fursa ya kuchagua chuo anachokitaka, iwapo ataweza kushindana na ushindani wa chuo husika na kuwataka watakaokwamishwa wawasiliane na TCU.

Prof. Kihampa alisema zipo changamoto za waombaji kuwa wapya, ila isitokee chuo kushiriki kukwamisha maombi ya mwanafunzi.

“Yoyote ambaye amepata udahili katika vyuo zaidi ya kimoja ana uhuru wa kufanya udahili kwenye chuo anachokitaka na isitokee kukwamishwa na mtu yoyote,” alisisitiza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Elimu

Viwanda zaidi ya 200 kuonyesha bidhaa maonyesho ya TIMEXPO Dar

Spread the loveSHIRIKISHO la Wenye Viwanda Nchini (CTI) kwa kushirikiana na Mamlaka...

Elimu

Wazazi wa wanafunzi waliokosa nafasi vyuo vikuu waonyeshwa njia na GEL

Spread the loveWAKALA wa Elimu ya Vyuo Vikuu Nje ya Nchi, Global Education...

ElimuHabari Mchanganyiko

Wanafunzi Nyamkumbu wanolewa na GGML kuhusu taaluma ya madini

Spread the loveZAIDI ya Wanafunzi 50 kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana...

Elimu

Green Acres kuwakatia bima wanafunzi wote

Spread the loveShule ya Green Acres imejipanga kufanya mambo makubwa kwa mwaka...

error: Content is protected !!