Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Wabunge waibana Serikali kikokotoo cha mafao, wataka muswada sheria ifutwe
Habari za SiasaTangulizi

Wabunge waibana Serikali kikokotoo cha mafao, wataka muswada sheria ifutwe

Patrobas Katambi
Spread the love

WABUNGE leo Jumanne wameitaka Serikali kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya Sheria hifadhi ya jamii ya mwaka 2017 ili iruhusu wastaafu kulipwa kwa mkupuo mafao yao kwa asilimia 100. Anaripoti Mlelwa Kiwale, TUDARCo…(endelea).

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wastaafu kutokana na kikokotoo hicho kipya kilichoanza kutumika Juni mwaka jana ambapo kwa mafao ya mkupuo mstaafu hupokea asilimia 33 ya mafao yake ilihali wabunge wakitaka wastaafu asilimia 100.

Hayo yamejiri leo bungeni jijini Dodoma wakati Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo (CCM) aliyehoji ni nini mpango wa serikali kuhusu malalamiko ya wastaafu juu ya kikokotoo kinachotumika kupiga mahesabu na kulipa mafao yao.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri huyo, amesema mpango wa serikali ni kuendelea kuelimisha wananchi hususani waajiri na wanachama ya mifuko ya pensheni ikiwemo wastaafu kuhusu faida na kanuni mpya ya mafao ya pensheni.

Amesema serikali kupitia mifuko ya pensheni na kwakushirikiana na Shirikisho la Vyama la Wafanyakazi (TUCTA) imejipanga na inaendelea kutoa elimu ya kanuni mpya zilizopitishwa Julai mosi mwaka jana na hadi kufikia tarehe 30  Juni 2023 mifuko ilitoa elimu kwa jumla ya waajiri 5,580 kati ya waajiri 6,200 waliopangwa kufikiwa katika kipindi hicho.

Ester Bulaya

Katika maswali la nyongeza, Tarimo alihoji Je, ni serikali imejipangaje hata hicho kiasi kinachotolewa sasa kitolewe kwa wakati lakini pia nini mpango wa serikali kuhakikisha wastaafu wanaopokea kiasi cha chini ya Sh 100,000 kwa mwezi nao kuongezewa pensheni ya mwezi.

Akijibu maswali hayo, Katambi aliendelea kusisitiza kuendelea kutoa elimu na kudai kuwa katika utafiti walioufanya asilimia 81 ya wanachama wananufaika na mafao ya mkupuo huo na kwamba mpango huo sasa una faida kuliko hasara.

Mbunge wa Viti Maalumu CCM, Mariam Kisangi naye alihoji uwapo wa walimu waliokumbwa na mfumo wa kikokotoo katika kipindi kilipoanza kutumika kwamba mpaka sasa mfumo wao wa pensheni haueleweki na haupo sawa.

Katambi alijibu kuwa utaratibu huo wa kuunganisha mifuko na kutengeneza uwiano sawa wa malipo haukuacha kundi lolote nje hivyo kama kuna  kundi la walimu limeachwa ataenda kulifanyia kazi kwa sababu mfumo haujabagua kundi lolote.

Mbunge wa Viti maalumu Chadema, Ester Bulaya alihoji ni lini serikali italeta muswada wa sheria hiyo bungeni ili wastaafu walipate japo asilimia 50 ya mafao yao ili waweze kujikimu.

Aliongeza kuwa lalamiko kubwa ni mafao ya mkupuo ambayo serikali imetoa asilimia 50 hadi 33 na sasa mstaafu ambaye angepaswa kulipwa Sh milioni 100 analipwa milioni 50.

Katambi aliendelea kujitetea kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu suala hilo la mafao hasa baada ya mifuko kuunganishwa.

“Awali kila mfuko ulikuwa na aina yake utoaji wa mafao, lakini kwa hatua ya sasa badala ya mkupuo ule wa asilimia 25, sasa imefikia asilimia 33 ya ulipaji wa mkupuo mafao hayo.

Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo

Mbunge wa Sumve, Kasalali Mageni (CCM) aligongea msumari katika swali la Bulaya kwamba kiuhalisi kikokotoo hicho kipya watumishi na wastaafu, hawakitaki.

“Ni lini serikali italeta muswada wa kufuta kikokotoo hiki ili kuondoa kero kwa watumishi na wastaafu ambao hawakitaki? Alihoji.

Kutokana na wabunge hao kuendelea kuchachambaa, Katambi alitumia msamiati kuwa hauwezi kuzungumza bila kufanya utafiti, hivyo akanukuu utafiti Serikali iliyoufanya kwamba katika ripoti yake inaonesha unufaika ni asilimia 81 ya wanachama wote.

Amesema kama kuna mtu (mbunge) ana hoja awafuate mawaziri husika na kuwaeleza shida yake lakini pia wataendelea kutoa elimu.

“Tunaona umuhimu wa kuweka semina kwa ajili ya wabunge kupata uelewa wa pamoja kuliko kuwapotosha,” amesema.

Spika wa Bunge Dk. Tulia Ackson naye alisisitiza wabunge wenye hoja kuhusu changamoto za mafao wawafuate mawaziri husika ili kupata suluhu ya changamoto za wapiga kura wao majimboni.

“Zile hoja za jumla ya kuendelea kutoa mafunzo ni muhimu kwa sababu hifadhi ya jamii inatakiwa kuonekana kuwa hifadhi ya jamii lakini ikionekana ni pesa ya uwekezaji wakati ni ya wastaafu inaleta changamoto kwa hiyo endeleeni kuelimisha jamii wajue nini wanapaswa kufanya na hizo pesa zinazotunzwa ni kwa ajili ya nini,” amesisitiza Dk. Tulia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde aibana kampuni kutimiza masharti ya mkataba

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameitaka Kampuni ya Xin Tai...

Habari za Siasa

Sauti ya Watanzania waeleza sababu za kuiunga mkono Chadema

Spread the love  KIKUNDI kinachojipambanua katika kupigania rasilimali na uhuru wa nchi,...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jacob, Malisa waachiwa kwa masharti

Spread the love  JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,...

Habari za SiasaKimataifaTangulizi

Tanzania, Somalia kuibua maeneo mapya ya ushirikiano

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Somalia...

error: Content is protected !!