May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

STAMICO, BUCKREEF wasaini mkataba wa uchorongaji wa Sh. bil 4

Spread the love

 

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limesaini mkataba wa uchorongaji na Mgodi wa Madini wa Buckreef (Buckreef Gold Company Ltd) ambayo ni kampuni inayochimba madini ya dhahabu katika mkoa wa Geita. Anaripoti Noela Shila, TUDARCo … (endelea).

Mkataba huo wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni nne, utadumu kwa muda wa mwaka mmoja.

Akizungumza katika hafla ya kusaini kandarasi hiyo leo tarehe 30 Agosti, 2021 jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Dk. Venance Mwasse amesema mkataba huo utahusisha mitambo ya kisasa ya STAMICO ya uchorongaji ya Diamond Drilling (DD) na Reverse Circulation (RC).

Amesema jukumu hilo la uchorongaji ni ya mwazo na utahusisha uchorongaji wa mita 10,000 za awali.

Amesema mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha 2021.

“STAMICO linamiliki mitambo mipya mitatu ya kisasa ya uchorongaji yenye uwezo wa kutoa huduma ya uchorongaji kwa wateja wake kwa haraka zaidi na kwa viwango vya juu zaidi kiushindani.

“Kufuatia utiaji saini wa mkataba huo na kuanza kazi Shirika linatarajiwa kutoa ajira za muda mfupi kwa wakazi wazawa na kuchangia uchumi wa wilaya ya Geita na taifa kwa ujumla,” amesema.

Amesema shirika linatoa wito kwa wachimbaji wadogo kujikita katika uchimbaji wa kisasa unaozingatia usalama migodini na utunzaji wa mazingira.

“Tunaipogeza Kampuni ya Buckreef kupitia Mkurugezi Khalaf Rashid kwa kuiamini STAMICO kufanya kazi hii ya uchorongaji. “Shirika linaahidi kufanya kazi kwa bidii na uweledi mkubwa ili kutoa matokea yenye tija kwa kuwa ina mitambo ya kisasa na wataalamu wa kutosha.

“Shirika linatoa wito kwa wamiliki wa migodi na makampuni mengine nchini kutumia mitambo ya kisasa ya uchorongaji kutoka Shirika la madini la Taifa, kwani lina uwezo, wataalamu na vifaa vya kufanya kazi ya uchorogaji,” amesema.

Aidha, Mkurugenzi wa Kampuni ya Buckreef, Khalaf Rashid ameishukuru Stamico kwa kuendelea kushirikiana pamoja katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika kuinua sekta ya madini nchini.

Wakati mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjilwa mbali na kuipongeza Stamico kwa miradi mbalimbali ya kimkakati iliyofanikiwa kuitekeleza, pia alilitaka Shirika hilo kuendelea kujiimarisha na kumiliki mgodi wake binafsi kwa asilimia 100.

Amesema mkataba huo uchorongaji ni mwendelezo wa kazi nzuri zinazofanywa na STamico kwani mwaka jana Stamico ilipata zabuni ya kuchoronga na kutafiti madini kutoka kampuni ya madini ya Geita Gold Mine Ltd. (GGML) wenye thamani ya Sh bilioni tisa.

“Ubora wa kazi zenu ndio unawafanya muendelee kupata zabuni nyingine kubwa na nzuri, Serikali tutaendelea kuwaunga mkono kwa sababu hata sasa utegemezi wa Stamico kwa serikali ni mdogo.

“Tutaendelea kuwaunga mkono hadi utegemezi uishe lakini pia kuhakikisha shirika linaendelea kutoa gawio kwa serikali kama mlivyoanza mwaka huu

“Shirika lilikuwa limekufa na lilitaka kufutwa kabisa lakini katika uongozi wa sasa ndani ya kipindi cha miaka mine mmefanikiwa kulifufua,” amesema.

error: Content is protected !!