JAMHURI ya Shirikisho la Somalia, imekubaliwa rasmi kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Uamuzi wa EAC kukubali ombi la uanachama wa Somalia, umetangazwa leo tarehe 24 Novemba 2023 na Mwenyekiti wa jumuiya hiyo anayemaliza muda wake, Evariste Ndayishimiye, katika mkutano wa 23 wa kawaida wa wakuu wa nchi za Afrika Mashariki, jijini Arusha.
Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, alikuwepo wakati Ndayishimiye ambaye ni Rais wa Burundi, anatangaza uamuzi huo.
“Kuhusu maombi ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, tumeamua kukubali ombi la Somali la kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Rais Ndayishimiye.
Ofisi ya Rais wa Somalia, kupitia ukurasa wake wa Twitter, mapema baada ya uamuzi huo kutangazwa, ilishukuru kwa taifa hilo kukubaliwa kujiunga katika jumuiya hiyo, huku ikiahidi kutoa ushirikiano kwa nchi wanachama katika kuleta ustawi na maendeleo.
“Ni siku ya kihistoria kwa Somalia katika mkutano wa 23 wa wakuu wa EAC mjini Arusha, Tanzania. Jamhuri ya Shirikisho la Somalia ina heshima kubwa ya kujiunga na jumuiya kama mwanachama wa nane, kuashiria enzi mpya ya matumaini na ustawi wa pamoja katika kanda,” imeandika ofisi hiyo.
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Rais wa Kenya, William Ruto, aliipongeza Somalia kwa kuwa mwanachama, huku akisema EAC imeongeza idadi ya watu milioni 15.
“EAC tulikuwa saba sasa ziko nchi nane, mniruhusu kuipongeza Jamhuri ya Shirikisho la Somalia kwa kujiunga na EAC na sasa tuna ziada ya watu milioni 15 ambao watakaokuja kuwa wanachama wa hii familia kubwa,” amesema Rais Ruto.
Nchi nyingine wanachama wa EAC ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Demokrasia ya Congo na Sudan Kusini.
Leave a comment