October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Vikawe wamuangukia Aweso utata mradi wa maji

Waziri wa Maji, Juma Aweso

Spread the love

BAADHI ya wananchi wa Mtaa wa Vikawe Shule, Kata ya Pangani, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wamemuomba Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuingilia kati usambazaji wa maji  kwenye mradi unaojengwa na Kampuni ya Ainan International ya China. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani… (endelea)

Wananchi hao wamesema wanaamini Waziri Aweso anaweza kumaliza sintofahamu iliyogubika mradi huo.

Wakizungumza juzi kwenye kikao kilichohudhuriwa na Balozi wa Shina No 1 wa Mtaa wa Vikawe Shule, Mhoja Omary wananchi hao walidai kuwa mchoro wa ramani ya awali unaoonyesha maeneo yote ambayo yamezungukwa na tenki kubwa la maji ya mradi huo  yangefikiwa.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza ramani hiyo imepotea katika mazingira tata, hivyo wanaamini kuna mchezo mchafu umefanyika.

Pia wananchi hao wanaitupia lawama Ofisi ya Serikali ya Mtaa kuwa chanzo cha tatizo hilo kutokana na usiri mkubwa uliopo.

Baadhi ya wananchi wa Shina No 1, Mtaa wa Vikawe Shule, Kata ya Pangani, Wilaya ya Kibaha Mkoa waPwani wakiwa kwenye kikao cha kujadili sintofahamu iliyogubika mradi wa maji unaoendelea kwenye mtaa wao.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia juzi umati wa wananchi waliokwenda Ofisi za Serikali ya mtaa huo ili kupata majawabu ya suala hilo.

Hata hivyo, hakuna kiongozi yeyote wa mtaa aliyekuwa tayari kuzungumza na wananchi hao.

Mmoja wa wazee hao Rajabu Athuman alisema anashangazwa na usiri uliogubika mradi huo akisema huenda kuna vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watu wenye fedha.

“Viongozi wa mtaa tukiwafuata hawana majibu, tunaambiwa ramani ya awali imefutwa na iliyopo sasa inatubagua, miundombinu yote tunaona wanapelekewa matajiri ambao wengine hata nyumba zao ziko porini na hazijaisha lakini tunaona mabomba na mitaro mikubwa inaelekezwa huko kwa matajiri na sisi tumeachwa.

“Awali ramani iliainisha Vikawe  Shule yote tutasambaziwa maji, leo hii tunaona kazi inaendelea maeneo mengine sisi ambao tumekaribiana kabisa na hanzo cha mradi (tanki) tunaachwa, hili halikubaliki, tunamuomba Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aje hapa tumweleze kilio chetu kwamba kwa nini tukose maji wakati tenki limejengwa kwetu? alihoji.

Mwananchi mwingine, Neema John alisema wananchi wote ambao mradi huo unaelekea kuwabagua walikwishapimiwa maeneo yao na wataalam wa maji lakini wanashangazwa kuambiwa kuwa hawamo kwenye ramani.

MwanaHalisi Online lilimtafuta Balozi wa Shina No 1 Mtaa wa Vikawe, Mhoja Omary alikiri kuwapo sintofahamu ya mradi huo.

Mhoja alisema amekuwa akifuatilia suala la maji katika eneo hilo kwa muda mrefu lakini anashangaa haoni miundombinu yoyote ya mabomba yanayotandazwa katika eneo lake analoliongoza.

“Nimekuwa nikifuatilia mradi huu kwa muda mrefu, nimeongea na Saveya wa maji nikaambiwa ramani ya sasa haionyeshi kama wananchi wa Mtaa wa Vikawe Shule watafikiwa na mradi huo, ni kinyume na makubaliano ya awali.

“Hata hivyo, wananchi karibu wote tunashangaa ramani yetu ya awali imekwenda wapi? alihoji.

Aidha, MwanaHalisi Online pia lilimtafuta Mwenyekiti wa Mtaa wa Vikawe Shule, Said Linji ili azungumzie suala hilo ambapo alisema hajui ni kilomenta ngapi za mtandao wa mabomba ya maji zinazotekelezwa katika mtaa wake hivyo aulizwe mkandarasi wa mradi husika.

” Ni kweli wananchi wameanza kuwa na wasiwasi kuhusu ufikiwaji wa mradi huo, kuhusu ramani siwezi kulisemea kwa sababu hata mimi siijui.

“Siwezi kudanganya sijui ni kilometa wala ukubwa wa huu mradi, hata sisi viongozi ramani iliyopo haituridhishi ingawa mimi si mtaalam wa vitu hivi” alisema Linji.

Meneja wa DAWASA Wilaya ya Kibaha, alipoulizwa alimtaka mwandishi  kuwasiliana na Meneja wa mradi huo, Valentine Njau.

Hata hivyo, Njau alisema hawezi kuzungumzia mradi huo kwakuwa si Msemaji wa DAWASA.

Alipotafutwa Msemaji wa DAWASA, Evarlasting Lyaro aliahidi kuwasiliana na Njau na atatoa majibu baadaye.

error: Content is protected !!