MKOA wa Shinyanga umeahidi kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Shirika la Legal Services Facility (LSF), katika utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga…(endelea).
Ahadi hiyo ilitolewa jana Jumapili na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme, katika uzinduzi wa kampeni hiyo inayofahamika kwa jina la Mama Samia Legal Aid Campaign, mkoani humo.
Mndeme ameagiza watendaji na viongozi wa kata za Shinyanga kutenga maeneo yatakayotumiwa na watoa msaada wa kisheria wakati wa utekelezaji wa kampeni hiyo hasa maeneo ya pembezoni.
Kampeni ya Mama Samia Legal Aid, inatarajiwa kufanyia Shinyanga kuanzia tarehe 11 hadi 21 Juni 2023.
“Kwa mara nyingine tena, ninatoa wito kwamba sisi sote tushikamane katika kumuunga mkono Kiongozi wetu, Dk. Samia Suluhu Hassani, katika kuondoa kadhia na viashiria vyote vya kuminya upatikanaji wa haki hususan ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ambayo ndiyo changamoto kubwa ya Mkoa wa Shinyanga,” alisema Mndeme.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul, alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine imedhamiria kuhakikisha kampeni hiyo inawafikia wananchi wote wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema kampeni hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha haki za binadamu na utawala Bora.
“Huduma ya msaada wa kisheria kuwafikia wananchi bure ni mapenzi na upendo mkubwa wa Rais Samia kwa mwananchi wa hali ya chini,” alisema Gekul.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Marry Makondo, alisema kampeni hiyo itasaidia kushighilikia masuala yote ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi na wosia, pamoja na kuelimisha Jamii kuhusu haki na wajibu wao kisheria na kikatiba.
Meneja Rasilimali na Mawasiliano kutoka LSF, Jane Matinde, alisema uzinduzi huo unakwenda kufanyika kila mkoa, huku ukienda sambamba na utoaji wa huuduma
za msaada wa kisheria ili kuchochea upatikanaji wa haki kwa wananchi hasa wasiojiweza ikiwemo wanawake, watoto na makundi maalum.
Leave a comment