December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

‘Sangoma’ wanne wauawa kisa mate

Sehemu ya vifaa vya waganga wapiga ramli

Spread the love

 

WANAKIJIJI wanne wakongwe wameteketezwa kwa moto jana tarehe 17 Oktoba, 2021 baada ya kutuhumiwa kuwa ni wachawi. Anaripoti Mwandishi Wetu  … (endelea).

Vikongwe hao waliuawa katika kijiji cha Nyagonyi, eneo la Marani Kisii nchini Kenya kufuatia tukio la utekaji nyara wa mwanafunzi wa shule ya sekondari ambaye alikutwa barabarani akiwa amepoteza fahamu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi eneo hilo la Kisii, Francis Kooli iliwataja marehemu hao kuwa Jemima Mironga (60), Agnes Ototo (57), Sigara Onkware (62) na Sindege Mayaka (85).

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwanafunzi huyo ambaye hapo awali alionekana mdhaifu alikuwa ametekwa nyara usiku wa kuamkia jana katika hali ya kutatanishi.

Wanakijiji walipomtemea mate alirejesha fahamu, akaanza kuzungumza na kuibua kizaazaa kikubwa pale alipowataja vikongwe hao waliodaiwa wachawi.

Watuhumiwa watatu kati ya walioteketezwa walikuwa wanawake ilhali mmoja alikuwa mwanaume mwenye umri wa takriban miaka 85.

Polisi walisema walipofika katika eneo la tukio walikuta tayari watu hao walikuwa wamekwishateketezwa.

Wakazi eneo hilo walidai watuhumiwa hao walioteketezwa walikuwa miongoni mwa genge la wachawi ambao walimdanganya mwanafunzi huyo wa shule ya sekondari ya Nyagonyi na kumtorosha shuleni hapo usiku wa Jumamosi.

Wanakijiji walisema kuwa mwanafunzi huyo alikuwa amerogwa na hali yake kudhoofu kila mara.

“Hata wazazi wake wameuza kila kitu ili kugharamia matibabu yake.

“Nadhani hii ni mara ya nne kama sio ya tano ambapo wanamteka nyara” alisema mmoja wa, wakazi aliyejitambulisha kama John Getuma.

Wanawake wawili kati ya washukiwa hao wanne waliwashutumu wenzao wawili lakini papo hapo walikuwa wa kwanza kuteketezwa.

Mwanamke wa tatu alivutwa kutoka nyumbani kwake ambako alikuwa amejifungia na kuteketezwa pamoja na nyumba yake.

“Mwanzoni hatukujua kilichokuwa kimefanyika lakini wakati nilienda karibu tulikuta mvulana akiwa amelala chini. Kila mtu aliagizwa amtemee mate. Tulipomtemea mate, alianza kuzungumza na hapo ndipo wanawake wale walichukuliwa na kuteketezwa” alisema mkazi mwingine aliyejitambulisha kama Moraa.

Vijana waliodaiwa kuwa walikuwa wamejihami waliendeleza msako kusaka wachawi wengine katika kijiji hicho.

Hata hivyo, polisi walisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo pia wameonya hatua hiyo na kuwataka wananchi hao kutojichukulia sheria mkononi.

error: Content is protected !!