June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia awapa ujumbe wapinga chanjo ya Korona

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka watu wanaopinga chanjo ya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19), wakajifunze katika mikoa iliyoathirika na janga hilo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kiongozi huyo wa Tanzania, ametoa wito huo leo Jumatano, tarehe 28 Julai 2021, katika uzinduzi wa chanjo ya UVIKO-19, uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Samia ametaja mikoa iliyoathirika na UVIKO-19 ni, Kilimanjaro, Arusha, Kagera na Dar es Salaam.

Amesema watu waliobuka na kupinga mpango wa Serikali wa kutoa chanjo, hawajaguswa na madhara ya janga hilo.

“Kwa wale ambao koo zao hazijaguswa, hawajapata madhara ya maradhi haya wanaweza kusema wanavyotaka. Lakini nenda leo Moshi (Kilimanjaro), nenda Arusha, Kagera hata Dar es Salaam, uonenae na zile koo ambazo wameshaguswa na haya maradhi. Wana maneno ya kukuambia,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema, familia zilizoguswa na ugonjwa huo, ikiwemo kwa kupoteza ndugu zao kutokana na UVIKO-19, wanatamani kuchanjwa chanjo hiyo.

“Na kama wangeweza, wangekuwepo leo kuchanja kutokana na madhara waliyopata,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewataka Watanzania wasipotoshe, juu ya zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO-19.

“Sasa ndugu zangu kabla hujapatwa na janga, unaweza kusema vyovyote. Lakini likikugusa unajua hatari ya hili janga. Naomba sana tusivunjane moyo, lakini tupeane moyo katika kupigana na janga ambao limeteremka duniani,” amesema Rais Samia.

error: Content is protected !!