June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia afungua dimba chanjo ya Korona

Rais Samia Suluhu Hassan akichanjwa chanjo ya korona

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amezindua zoezi la utoaji chanjo ya Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19), kwa kuchanjwa aina ya Johnson & Johnson. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia amechanjwa chanjo hiyo leo Jumatano, tarehe 28 Julai 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya kuchanjwa chanjo hiyo, Rais Samia amesema amekubali kupata afua hiyo, kwa kuwa haina madhara.

“Mimi ni mama wa watoto wanne wanaonitegema, ni bibi wa wajukuu kadhaa wanaonipenda na nawapenda sana. Ni mke, lakini mbali ya yote ni rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Nchi, nisingejitoa mwenyewe, nisingejipeleka kwenye kifo na hatari nikijua nina majukumu yanayotegemea,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameongeza “Lakini nimetoka kuonesha umma na wanaonifuata nyuma nikijua kwamba rais ni mchungaji, nina watu nyuma. Kwa hiyo nisingetoka kujihatarisha. Nimekubali nikijua ndani ya mwili wangu nina chanjo nimeishi nazo kwa miaka 61.”

Rais Samia amesema, chanjo hizo sio hatari kama inavyodaiwa na baadhi ya watu “sioni hatari iliyoko na baada ya wanasayansi kujiridhisha duniani, zimekuja nchini wanasayansi wetu wamejiridhisha.”

Rais Samia amesema, chanjo hiyo ni hiari na wala hakuna mwananchi atakayelazimishwa kuipata, ingawa amehimiza wachanjwe kwa ajili ya kuokoa maisha yao.

“Chanjo ni hiari ya mtu na imani, inanikumbusha miaka ya 1960 wakati tuko shule msingi tulichanjwa chanjo. Na niseme kwenye mwili wangu nina chanjo tano na ya leo ya sita, nimekuwa nikiishi nazo na zimenipa uzima wa kutosha mpaka leo nimefika hapa,” amesema Rais Samia.

Mbali na Rais Samia, wengine waliopata chanjo hiyo ni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mke wake, Marry. Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga.

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama waliopata chanjo hiyo ni, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo. Inspekta Jenerali wa Polisi nchini, IGP, Simon Sirro na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala.

Wengine ni, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima.

error: Content is protected !!