October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia ataja sababu kushiriki mkutano UN

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema ameamua kushiriki mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), kwa kuwa katika kipindi cha miaka sita nchi ilikuwa inatuma wawakilishi badala ya kiongozi wa nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumamosi, tarehe 25 Septemba 2021, akihutubia nchi baada ya kurejea akitokea nchini Marekani, alikokuwa kwa ziara ya kikazi tangu tarehe 19 Septemba mwaka huu.

“Tumekwenda kwenye safari ambayo kwa miaka sita tumekuwa tukiwakilishwa katika ngazi ya uwaziri na ubalozi, lakini hatukwenda kama kiongozi wa nchi. Lakini mara hii tumeweza, tumekwenda, tumeshiriki na wenzetu na dunia inawasalimia,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema ziara yake hiyo ilizaa matunda kwa kuwa alipata nafasi ya kuzungumza na viongozi mbalimbali, ikiwemo Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles Michel na wafanyabiashara wa Marekani waliowekeza na wanaotaka kuwekeza Tanzania.

“Katika mkutano huo tulipata fursa ya kuonana na watu mbalimbali, nilionana na Rais wa Benki ya Dunia, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Biashara duniani, nilionana na wafanyabaishara wa Marekani waliowekeza Tanzania na wanaoataka kuja. Nilionana na marais kadhaa wenzangu,” amesema Rais Samia.

Akizungumzia hotuba yake aliyoitoa juzi Alhamisi katika mkutano wa UNGA, Rais Samia amesema alitumia jukwaa hilo kuzungumzia mambo manne, ikiwemo masuala ya kiuchumi, Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19), utalawa bora na mazingira.

“Kwa niaba yenu ndugu zangu niliahidi Umoja wa Mataifa kwamba, Tanzania tutayafanyia kazi yote haya ili nasi twende na dunia inavyokwenda,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amewaomba Watanzania wamuunge mkono katika kutekeleza yale aliyoyaahidi kwenye mkutano huo.

“Lakini niseme kwamba, kuzungumza kwenye taasisi kama ile ni jambo moja, la pili ni utekelezaji wa yale niliyoyazungumza, niwaombe Watanzania wote tuungane, tushirikiane na tufanye kazi kwa pamoja kujenga taifa letu,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Taifa ambalo kwa miaka 60 sasa limekuwa likijengwa kwa awamu na hatua mbalimbali, kila awamu imekuwa ikiweka matofali katika kujenga taifa. Niwaomba tujenge kwa matofali madhubuti ili tuweze kulisimamisha vyema taifa letu.”

error: Content is protected !!