Friday , 3 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz
Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the love

Wakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi kufikia Dola za Kimarekani bilioni moja (Sh trilioni 2.5), ndani ya mwaka mmoja Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza majadiliano na ushirikiano ulioanzishwa katika Kongamano la Biashara la Tanzania na Uturuki mjini Istanbul, utafungua njia kwa jumuiya za wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili kutumia fursa zilizopo kufikia malengo hayo. Anaripoti Gabriel Mushi, Instabul- Uturuki… (endelea).

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafanyabiashara na wawekezaji katika Jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Uturuki lililofanyika Jijini Istanbul tarehe 19 Aprili 2024.

Kwa sasa, kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Uturuki kinafikia dola za Kimarekani milioni 350 kwa mwaka.

Katika mkutano wao mjini Ankara juzi Alhamisi, Rais Samia na mwenzake wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, walikubaliana kuongeza kiwango cha biashara kufikia dola za Marekani bilioni moja.

Akizindua kongamano hilo lililowakutanisha wafanyabiashara zaidi ya 100 wa Tanzania na wengine zaidi ya 200 kutoka Uturuki jana Ijumaa mjini Istanbul, Rais Samia aliwahimiza wawekezaji wa Uturuki kutumia fursa zilizopo katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki, zikiwemo sekta za kilimo, utalii na viwanda.

Alisema Tanzania yenye zaidi ya watu milioni 60 huku asilimia 65 wakiwa ni vijana wenye umri chini ya miaka 30, ni eneo la kimkakati kama lango la ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, ambalo linajumuisha soko la watu wapatao milioni 500.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Cevdet Yilmaz akizungumza na wafanyabiashara na wawekezaji hao.

“Tanzania ni nchi yenye fursa pana katika kuimarisha biashara zenu kutokana na uwepo wa bandari ikiwamo ya Dar es salaam ambayo inatoa huduma kwa nchi nane zinazoitegemea Tanzania hivyo ni eneo la kimkakati katika kuimarisha biashara na uwekezaji wenu,” Rais Samia alisema.

Akizungumzia ujenzi wa reli ya kisasa unaounganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Burundi, alisema mtandao huo wa reli unalenga kuimarisha usafirishaji wa mizigo mizito ya hadi tani 10,000.

Aidha, akizungumzia lengo la biashara kati ya nchi hizo kufikia dola za Marekani bilioni moja, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Dk Ashatu Kijaji alitoa wito kwa jumuiya za wafanyabiashara kutoka nchi zote mbili kushirikiana katika kuwekeza kwenye sekta ya viwanda na kilimo.

Dk. Kijaji alisema sera zilizopo sasa zimefungua milango ya biasharana uwekeza nchini.

“Uongozi bora uliopo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, na mageuzi yenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara ndio chachu ya kufikia lengo hili,” alisema.

Naye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Uturuki, Cevdet Yilmaz alisema ukubwa wa biashara uliopo hivi sasa kati ya nchi hizo mbili hauakisi uhalisia wa uhusiano wa pande mbili kati ya Dar es Salaam na Istanbul.

Alisema juhudi za pamoja zinatakiwa kuwekewa mikakati ili kufikia malengo yaliyoafikiwa na marais hao wawili.

Awali, Mkurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Theolbald Sabi, alibainisha kuwa uwiano wa sasa wa biashara umeegemea zaidi Uturuki kuliko Tanzania.

Alieleza kuwa uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili unaweza kuiwezesha Tanzania kuongeza mauzo ya nje na kuifanya Istanbul kuwa daraja la kufikia soko la Ulaya.

Rais Samia yuko katika ziara ya kiserikali ya siku tano nchini Uturuki.

Ziara hii, ambayo ni ya kwanza kufanywa na mkuu wa nchi wa Tanzania mjini Ankara katika kipindi cha miaka 14, inaangazia kuboresha ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!