RAIS Mstaafu wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, amesema demokrasia ya barani Afrika, inapitia changamoto nyingine, ambazo baadhi yake zinasababishwa na taasisi zinazosimamia suala hilo kuwa dhaifu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea).
Dk. Kikwete ametoa kauli hiyo leo tarehe 18 Julai 2023, akitoa masuala yaliyojadiliwa katika mkutano wa viongozi wastaafu Afrika kuhusu hatma ya demokrasia.
“Kumekuwepo na tatizo la demokrasia iliyokuwepo, chaguzi zina mashaka lakini pia katika uchambuzi imeonekana kwamba katika demokrasia ya Afrika ushiriki wa wanawake na vijana hauridhishi. Yako matatizo makubwa ya rushwa katika demokrasia zetu lakini udhaifu wa zile taasisi zinazosimamia demokrasia,” amesema Dk. Kikwete.
Mbali na taasisi zinazosimamia demokrasia kuwa dhaifu, Dk. Kikwete amesema changamoto nyingine inayorudisha nyuma maendeleo ya suala hilo ni rushwa na uroho wa madaraka, ambapo katika kipindi cha miaka nane bara hilo limeshuhudia mapinduzi ya kijeshi 21 katika mataifa tofauti.
“Kuna baadhi ya nchi zinapitia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kama ilivyo Sudan, hakuna mapinduzi lakini majenerali wawili wameamua kuvuruga nchi yao hata wanachopigania haijulikani. Mkishakuwa na mazingira hayo hata demokrasia haiwezekani,” amesema Dk. Kikwete.
Kufuatia changamoto hizo, Dk. Kikwete amesema viongozi wastaafu walioshiriki mkutano huo wametoa maazimio yao juu ya namna ya kuboresha demokrasia, ambayo yatawasilishwa katika Umoja wa Afrika (AU), kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Leave a comment