JESHI la Polisi nchini, limesema limeanza uchunguzi wa tukio la gari la Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, kushambuliwa na risasi na watu wasiojulikana, akiwa safarini kuelekea Arusha, akitokea jijini Dodoma. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa ya uchunguzi huo imetolewa leo tarehe 30 Juni 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, DCP David misime.
“Jeshi la Polisi limepokea taarifa ya mbunge wa Simanjiro na dereva wake wakiwa safarini, gari walilokuwa wanatumia kushambuliwa kwa risasi katika kijiji cha Ngaboko wilayani Kiteto na kwa bahati nzuri hakuna aliyepata madhara,” imesema taarifa ya Kamanda Misime na kuongeza:
“Polisi wanafuatilia tukio hilo kwa karibu sana kwani uchunguzi ulishaanza mara baada ya kupokea taarifa, timu ya wataalamu wa uchunguzi wa matukio yaliyohusisha matumizi ya risasi kutoka makao makuu imetumwa kwenda kushirikiana na timu ya mkoa wa Manyara kuchunguza tukio hilo ili kubaini waliohusika ni akina nani na madhumuni au kusudio lao lilikuwa ni nini.”
Tukio hilo linadaiwa kutokea jana wakati Ole Sendeka anarudi jimboni kwake kupitia njia ya Kiteto, ambapo gari aina ya Double Cabin Silver iliwafuatilia na baadae kuanza kuwafyatulia risasi kadhaa zilizoishia katika gari na kushindwa kuwaathiri waliokuwamo ndani.
Leave a comment