Monday , 6 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa NEC yateua 15 kugombea urais Tanzania
Habari za Siasa

NEC yateua 15 kugombea urais Tanzania

Tundu Lissu, Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, akirudisha fomu ya kuteuliwa nafasi hiyo kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage
Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewateua wagombea 15 kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Wagombea hao wameteuliwa leo Jumanne tarehe 25 Agosti 2020 na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage baada ya kuwasili ofisi za tume hiyo jijini Dodoma.

Kati ya vyama 17 vilivyochukua fomu, mgombea wa Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele hajateuliwa kugombea urais baada ya kushindwa kukidhi matakwa ya kikatiba na sheria.

Kati ya wagombea hao 15 walioteuliwa kupeperusha bendera ya vyama vyao, kuna wagombea wawili wanawake ambao ni Qeen Cuthbert Sendiga wa chama cha ADC na Cecilia Mwanga wa chama cha Demokrasia Makini.

John Magufuli, Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, akirudisha fomu ya kuteuliwa nafasi hiyo kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na wagombea wawili wanawake tangu ulipoanza uchaguzi wa kwanza ulioshiriki vyama vingi mwaka 1995.

Mwaka 2005, Anna Senkoro aligombea urais kupitia chama cha PPT-Maendeleo.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, kulikuwa na mwanamke mmoja ambaye ni, Anna Mghwira kupitia ACT-Wazalendo.

Kwa sasa Anna aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli.

Prof. Ibrahim Lipumba, Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CUF, akirudisha fomu ya kuteuliwa nafasi hiyo kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage

Idadi ya walioteuliwa kugombea urais ni kubwa na haijawahi kutokea tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 ulipoanza.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, waliochukua fomu walikuwa 11, nane walirejesha fomu na kuteuliwa na wawili hawakurejesha huku mmoja alirejesha nje ya muda uliokuwa umepangwa.

Kampeni za uchaguzi mkuu zinaanza kesho tarehe 26 Agosti na kuhitimishwa 27 Oktoba 2020 na siku inayofuata ya Jumatano 28 Oktoba 2020 itakuwa siku ya uchaguzi mkuu.

Hashim Rungwe, Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chaumma, akirudisha fomu ya kuteuliwa nafasi hiyo kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage

Wengine walioteuliwa ni; John Pombe Magufuli (CCM), Leopard Mahona (NRA), John Shibuda (Ada Tadea), Mutamwega Mgaiwa (SAU), Cecilia Augustino Mwanga (Demokrasia Makini), Yeremia Maganja (NCCR-Mageuzi) na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF.

Pia wamo, Philip John Fumbo (DP), Bernard Membe (ACT- Wazalendo), Qeen Cuthbert Sendiga (ADC), Twalib Ibrahim Kadege (UPDP), Hashimu Rungwe (Chaumma), Khalfan Mohamed Mazurui (UMD) na Seif Maalim Seif (AAFP).

Cecilia Augustino Mwanga, Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Demokrasia Makini, akirudisha fomu ya kuteuliwa nafasi hiyo kwa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage

Kuanzia leo Jumanne hadi kesho Jumatano tarehe 26 saa 10 jioni itakuwa mwisho kwa watu wanaotambulika kisheria kuweka pingamizi dhidi ya mgombea yoyote aliyeteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mbatia ambwaga Selasini, mahakama yaamuru alipwe fidia

Spread the loveMAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemuamuru...

Habari za SiasaTangulizi

Mkulo afariki dunia, kuzikwa kesho Kilosa

Spread the loveALIYEKUWA Waziri wa Fedha na Mbunge wa Kilosa (CCM), Mustafa...

Habari za SiasaTangulizi

Sabaya afutiwa kesi, ruksa kugombea uongozi

Spread the loveMwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali DPP leo Ijumaa amefuta rufaa...

Habari za Siasa

Serikali yasaka bilioni 3 kujenga daraja Mto Mpiji

Spread the loveSerikali imesema inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kiasi cha...

error: Content is protected !!