May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NEC : Jimbo la Konde liko wazi

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera

Spread the love

 

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza Jimbo la Konde visiwani Zanzibar, liko wazi baada ya mbunge wake mteule kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sheha Mpemba Faki, kujiuzulu kwa sababu za kifamilia. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa jana tarehe 2 Julai 2021 na Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk. Wilson Mahera, baada ya Faki kujuzulu nafasi hiyo.

Taarifa ya Mahera imesema kuwa, NEC imeamua kutangaza jimbo hilo kuwa wazi, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, juu ya uamuzi wa mwanachama wake kujiuzulu ubunge.

“NEC imepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM yenye Kumb. Na. CCM/T.40/8vol.1/72, ya tarehe 2 Agosti 2021, ikitoa taarifa kuwa Mbunge mteule wa Konde, Faki aliandika barua kwa chama hicho kukitaarifu kuwa hayupo tayari kuwawakilisha wananchi wa Konde katika Bunge , kutokana na changamoto za kifamilia,” imesema taarifa ya Dk. Mahera.

 

Sheha Mpemba Faki

Taarifa hiyo imesema, taratibu za kujaza nafasi hiyo zitatangazwa baadae.

“Kutokana na hatua hiyo, tume inatoa taarifa kwa umma kuwa Jimbo la Konde lipo wazi na taratibu za kujaza nafasi hiyo zitatangazwa hivi karibuni. Tume imefanya hivyo kwa kuwa ilikuwa bado haijamjulisha Spika wa Bunge, kuhusu kukamilika kwa uchaguzi huo na kuchaguliwa kwa Faki,” imesema taarifa ya Dk. Mahera.

Faki alijiuzulu nafasi hiyo siku 15 baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Konde, uliofanyika tarehe 18 Julai 2021, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Khatib Said Haji kupitia ACT-Wazalendo, kufariki dunia.

Katika uchaguzi huo, Faki alimbwaga aliyekuwa mgombea wa ACT-Wazalendo, Mohammed Said Issa.
Haji aliyeliongoza jimbo hilo kwa zaidi ya miaka 10 akiwa Chama cha Wananchi (CUF) na ACT-Wazalendo, alifariki dunia tarehe 20 Mei 2021, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa anapatiwa matibabu.

error: Content is protected !!