Saturday , 27 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Nani anaifisidi Z’bar?
Makala & Uchambuzi

Nani anaifisidi Z’bar?

Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar (kushoto) walipokuwa katika mazungumzo ya muafaka na Maalim Seif Shariff Hamad
Spread the love

NI jabari gani wa kuthubutu kujitokeza leo na akatamka hadharani kuwa, ameikosea Zanzibar kwa vitendo vyake vya kuifisidi kiuchumi? Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Swali hili waulizwe viongozi wakuu. Waulize mmoja baada ya mwengine; wakubwa kwa wadogo miongoni mwa viongozi.

Waulize wateule wa rais ambao kwa nafasi zao huitwa viongozi wa kisiasa. Waulizwe hivi, nyie mmefisidi uchumi wa wananchi, eti?

Waulize swali hilohilo watendaji wanaoshika idara na taasisi za serikali “eti kati yenu yupo yeyote ametenda dhambi kwa kujinufaisha binafsi kupitia nafasi aliyoteuliwa kuongoza?”

Ni nani huyo anayeweza kuonesha majuto kwamba ameitendea ubaya nchi hii ya visiwa vikubwa viwili na vingine kadhaa vidogo kote Unguja na Pemba?

Si rahisi kujitokeza mtu. Hakuna mwenye kifua akafanya hivyo. Na hatatokea yeyote yule hata ukipigwa upatu na zawadi kutangazwa.

Hatatokea mmoja akamfunga paka kengele katika janga hili; utadhani hakuna aliyetenda dhambi kwa mgongo wa kuitumikia nchi hii.

Hata wale wanaofasidi bado wanasimama na kujinasibu kuwa, wanaipenda Zanzibar; wanaionea huruma na hawawezi kuihujumu kwa sababu wao ni wazalendo kwelikweli.

Usije ukathubutu kuwaamini. Kwamba ukiwasikia huku ukishuhudia macho yao na mwili wa kila mmoja wao anapozungumza kuhusu uadilifu wake, basi uamini viapo vyao eti ni wasafi. Hakuna kitu kama hicho.

Vuta subira nikwambie uchafu wa baadhi ya viongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baadhi yao hawafai hata kupewa kuongoza shehia. Ni kwanini hawafai?

Kwa sababu wananuka uvundo na hawasafishiki kwa sabuni unayoijua; isipokuwa kwa kukamatwa na kushitakiwa kwenye mahakama ya kisheria.

Wakamatwe na chombo cha ukamataji – Jeshi la Polisi ambacho kipo kikatiba na ndicho kimepewa jukumu la kuchunguza, kukamata na kumpeleka mshukiwa mahakamani.

Na kwa kuwa makosa ya watendaji hao na washirika wao yanahusu kula rushwa, kufisidi na kuhujumu nchi kiuchumi, wachunguzi wa Tume ya kukomesha rushwa na ufisadi wanapaswa kushiriki.

Lakini lipo swali jipya hapa la kuulizwa tena: Ni nani katika walioko safu ya juu kabisa ya uongozi Zanzibar aliye tayari kuona hatua hii muhimu inatekelezwa?

Naapa kwa jina la Allah aliyetuumba na kutandika ardhi na anga na vyote vinavyoishi, hayupo hata mmoja. Kama wote ni wachafu ama la, ni suala la kusubiri kuona.

Hebu Mzanzibari uliyepo ndani ya Zanzibar tenga muda uzunguke bandarini Malindi. Angaza macho kule mbele kama vile unaangalia kisiwa kidogo cha Prisoner.

Utaona vyombo kadha wa kadha. Si shida yako vyote hivyo. Unachotaka wewe ni kile chombo chenye umbo kubwa kuvishinda. Utakiona kipo pale kinaeleaelea.

Maji yanakisukuma na chenyewe kwa nguvu ya maji ya bahari, kinabarizi mawimbi kwa kwenda mara huku, mara kule. Cheupe, kirefu kiasi chake na kina ghorofa mbili. Ni kizuri kinachopendeza machoni.

Pembeni mwake utakuta kimebeba maneno “Mv Mapinduzi II.” Haya maneno yanawakilisha jina la chombo hiki mali ya umma.

Ni jina zuri kwa kweli ambalo linakupa kumbukumbu fulani. Kwamba ipo meli ya awali -Mv Mapinduzi. Hakika ilikuwepo ila hadithi yake nayo uvundo.

Hii Mv Mapinduzi II, kama ilivyokuwa ile ya kwanza iliyonunuliwa nchini Japan miaka ya 1980 ikiwa mpya, ilizinduliwa kwa shangwe na vigelegele vingi Disemba 3, 2016.

Ni meli iliyonunuliwa na serikali na umma ukaambiwa kuwa ni “meli mpya kabisa.” Ikaelezwa ilivyo kiufundi kama sehemu ya sifa zake nyingi. Meli imetengenezwa na wataalamu wabobezi wa nchini Korea Kusini.

Wakati inazinduliwa pale kwenye uso wa Bandari huku watu wakiiona fawahisha, si wengi walioitilia shaka meli hii kuhusu umadhubuti wake. Na kampeni ya kuitangaza kama isiyo makini na haikupata nguvu.

Nguvu za kuitaja Mv Mapinduzi II na sifa zake nyingi kama zilivyowekwa, zilikuwa kubwa kupindukia mpaka. Haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kuthubutu kutoa neno la kubadilisha mkao wa meza.

Ukubwa wake ulipaa sana kwa sababu uzinduzi wenyewe ulitumika kama sehemu ya mkakati kabambe wa kumrudisha kitini Dk. Ali Mohamed Shein.

Dk. Shein aliridhika kwa yote yaliyotanguliwa kuelezwa na wateule wake – Omar Yussuf Mzee aliyekuwa waziri mwenye dhamana ya fedha na muongoza Kamati ya ununuzi wa Meli hiyo.

Msemaji wa kwanza alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu. Wizara hizi mbili ndio wizara mama katika ushughulikiaji mipango ya kununua meli hiyo. Kulikuwa na Kamati ya kitaifa iliyoratibu utafutaji wa fedha za kununulia meli yenyewe.

Sasa fikiria wateule wa bwanamkubwa waliounda kamati iliyotarajiwa kutafuta fedha za kununua meli kubwa ya abiria na mizigo watoke na mikono safi baada ya kukamilisha jukumu hilo katika wakati ambao vyanzo vya mapato vilikuwa vikavu na serikali haijasimama.

Basi ndo hayo; meli iliyoitwa mpya ilitia nanga; uzinduzi ukafanywa kwa mbwembwe. Ila ililazimika kupelekwa chelezoni Mombasa kabla ya kuanza kazi.

Hiyo hasa ndiyo habari yenyewe ya ufisadi inavyoanzia maana sasa mwaka tu wa kuzunguka, meli haifanyi kazi.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!