Wednesday , 6 December 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Mzaha, mzaha, kazi iendelee
Makala & UchambuziTangulizi

Mzaha, mzaha, kazi iendelee

Spread the love

RIPOTI za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka wa fedha 2021/ 2022 zimejadiliwa bungeni. Je, umefurahishwa na mjadala? Je, kuna jipya?

Wakati wabunge wanajadili kwa mhemko mkubwa, mawaziri walikuwa wanachati; hawajali. Kwa nini? Kwa sababu ni mjadala uleule, wanaojadili ni walewale, hoja ni zilezile na matokeo yaleyale: kati yao hakuna atakayewajibishwa.

CAG Kichere


Ripoti ya CAG ni kati ya nyaraka muhimu za usimamizi makini wa fedha za umma na hutolewa kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni. Kikatiba, ripoti hizo zinapaswa kuwasilishwa kwanza kwa Rais kabla au kila Machi 30 na huwa na masuala muhimu yanayohusu fedha za umma yaani mapato na matumizi.

Ripoti huwasilishwa kwanza kwa Rais kwa sababu ndiye kiongozi mkuu wa nchi; ndiye huhangaika kukusanya fedha kutoka vyanzo mbalimbali vya ndani na nje. Rais ndiye huanzisha miradi ya kimkakati na kuvutia uwekezaji mkubwa.

Ukaguzi unalenga kujua ni kwa kiasi gani sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa fedha za umma zinafuatwa wakati wa matumizi.

Kwa bahati mbaya sana ripoti za CAG hazitiliwi maanani. Kazi ya CAG ni kuonesha fedha zilivyoliwa, zilivyofisidiwa, zilivyotumika kwa ubadhirifu. CAG hawezi kumshtaki yeyote na hakuna msaada kutoka Takukuru wenye uwezo wa kushtaki.

Joseph Msukuma

CAG anawasilisha ripoti bungeni Machi lakini inakuja kujadiliwa Novemba. Bado madudu ambayo wabunge walijadili mwaka jana ndiyo yamejirudi mwaka huu na hakuna hatua.

Ndiyo maana Joseph Kasheku, Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini (CCM) anasema “Kama Bunge tunaletewa hizi taarifa kwa ajili ya kuzungumza na kwenda nyumbani ni bora mkabadilisha utaratibu mkamalizana huko nje. Kwa sababu mimi najiuliza kila siku tunazungumza kitu kilekile.”

Anahoji, “Huyu KADICO ni nani. Mimi nataka kujua nyuma yake kuna nani…ni nani huyo au naye ni Chalinze; haina mwenyewe?” Tangu akiwa nje ya Bunge amekuwa akisikia mjadala kuhusu KADICO lakini hakuna hatua zinazochukuliwa.

Ripoti ya CAG mwaka 2013/ 2014 iliibua sakata la fedha za Escrow. CAG alisema fedha hizo ambazo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilikuwa linaweka katika akaunti ya Escrow kusubiri kumalizika mgogoro wa malipo kati yake na kampuni ya IPTL, zilikuwa mali ya serikali.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilisisitiza hivyo. Wabunge walijadili hivyo. Lakini mkuu wa nchi wakati huo Jakaya Kikwete alisema fedha hizo zilikuwa za IPTL. Hivyo kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 300 kikachukuliwa na IPTL badala ya serikali ili kusaidia kuliokoa kiuchumi shirika hilo lililokuwa likikabiliwa na ukata.

Nikwambie kitu. Serikali ya CCM haipendi kuadhibu mafisadi. Ndiyo maana aliyetajwa na CAG kusababisha upotevu wa fedha za polisi ameteuliwa kuwa balozi, na aliyetajwa kuweka kwenye akaunti tofauti fedha za “plea bargaining” kapandishwa cheo kuwa jaji.

Hata kule CCM, mtu aliyevamia Clouds Media kwa mabunduki ndiye msemaji mkubwa wa chama. Kazi iendelee.

Mwandishi wa Makala haya ni Joster Mwangulumbi anapatikana kwa simu namba 0753626751.

1 Comment

  • Sijui nani wa kulaumiwa mwezi wa tatu kujandiliwa mwezi wa kumi na moja..! Ripoti inaweka wazi mambo yote..! Atua inayo chukuliwa ni ‘0’..kweli? Sote tupo..kunani?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaTangulizi

Bei ya Dizeli, Petroli yashuka

Spread the loveBEI ya mafuta kwa mwezi Disemba, imeshuka kutokana na kupungua...

Habari za SiasaTangulizi

Chanzo maporomoko yaliyoua 65 Hanang, chatajwa

Spread the loveSERIKALI imesema kumeguka kwa sehemu ya Mlima Hanang ambao ilikuwa...

Habari za SiasaTangulizi

Maafa Manyara: Rais Samia akatisha ziara yake Dubai

Spread the loveRAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amekatisha ziara yake...

Habari za SiasaTangulizi

Wataalaam wa miamba watua Hanang

Spread the loveWaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na...

error: Content is protected !!