October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Muigizaji filamu maarufu wa Nigeria akamatwa

Spread the love

JESHI la Polisi nchini Nigeria, limethibitisha kumkamata mchezaji filamu maarufu nchini humo, Chiwetalu Agu kwa kuvaa vazi lenye bendera ya kikundi cha jamii ya wazawa ya watu wa Biafra (Igbo) kinachotaka kujitenga na kuchochea watu kujiunga nacho. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Jeshi linasema shuguli za Agu za kukinadi kikundi hicho ni kinyume cha sheria.
Kikundi hicho kinataka kujitenga katika jimbo la kusini-mashariki mwa Nigeria.

Kulingana na taarifa kutoka makao makuu ya jeshi, wamemkamata wakati walipokuwa wakifanya msako wa wafuasi wa genge linalounga mkono jamii ya wazawa ya Biafra wanaotaka kujitenga nchini humo (IGBO).

Imeelezwa mchezaji filamu huyo, alichukuliwa alipokuwa amevaa nguo zinazotambulisha kikundi hicho kwa ajili ya kumuhoji na ingawa alionesha pingamizi, jeshi limefanya juhudi za kumuweka mahabusu na linasema halikumyamyasa wala kumtesa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa ingawa jeshi linatambua haki za raia wote za kutembea kwa uhuru na kujieleza kama haki yao ya kikatiba, halitakubali ukiukaji wa wa sheria wa mtu binafsi au kikundi kwa kuchochea umma kufanya ghasia au kuvunja sheria na utulivu.

Kundi hilo linataka eneo fulani kusini-mashariki lenye watu kutoka kabila la Igbo, wajitenge na kuunda taifa lao huru la Biafra. Kundi hilo lilianzishwa mwaka 2014 na Nnamdi Kanu, ambaye alikamatwa na kukabiliwa na mashtaka ya ugaidi na uhaini.

error: Content is protected !!