October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Waliotemwa uwaziri, wapangiwa kamati za Bunge, Polepole ‘avuliwa’ uongozi

Dk. Faustin Ndungulile

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amefanya mabadiliko madogo ya wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge huku akiwapangia kamati waliokuwa mawaziri ambao wametenguliwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mabadiliko hayo, yametangazwa leo Jumamosi, tarehe 9 Oktoba 2021 na Ofisi ya Spika yakihusiaha wabunge saba wakiwemo waliokuwa mawaziri watatu ikiwa ni takribani siku 27 tangu Rais Samia Suluhu Hassan atengue uteuzi wao.

Rais Samia alifanya mabadiliko madogo ya baraza lake la mawaziri, tarehe 12 Septemba 2021 kwa kuteua mawaziri na wengine kutengua uteuzi wao.

Mawaziri hao waliotenguliwa ni, Dk. Leonard Chamuriho aliyekuwa waziri wa ujenzi na uchukuzi ambaye nafasi yake aliteuliwa Profesa Makame Mbarawa, sasa Dk. Chamuriho ameteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya sheria ndogo.

Dk. Faustine Ndugulile aliyekuwa waziri wa mawasiliano na teknolojia ya habari ambaye nafasi yake aliteuliwa Dk. Ashatu Kijaji. Dk. Ndugulile ambaye ni Mbunge wa Kigamboni ameteuliwa na Spika Ndugai kuwa mjumbe wa kamati ya sheria ndogo na kamati ya masuala ya UKIMWI.

Dk. Medard Kalemani

Mwingine ni aliyekuwa waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ambaye nafasi yake aliteuliwa na Janaury Makamba, sasa Dk. Kalemani ambaye ni Mbunge wa Chato amepangiwa kamati ya sheria ndogo.

Aidha, Spika Ndugai amemhamisha kamati ya Bunge, Humphrey Polepole aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya utawala na serikali za mitaa kwenda kamati ya sheria ndogo.

Kuhamishwa kwa Polepole kunamfanya kupoteza nafasi yake ya uongozi wa kamati uliokuwa unamfanya kuwa mjumbe wa Kamati ya Uongozi inayohusisha wenyeviti wote wa kamati za kudumu za Bunge ambapo mwenyekiti wake ni Spika.

Polepole ameondolewa uongozi wa kamati kipindi ambacho suala la hatima yake haijawekwa wazi baada ya kuhojiwa na kamati ya maadili ya chama chake- Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Humphrey Polepole, Mbunge wa Kuteuliwa

Mbali na Polepole aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM kuhojiwa, wengine ni, wabunge wenzake wa chama hicho, Jerry Silaa (Ukonga) na Askofu Josephat Gwajima (Kawe) ambapo taarifa yao imewasilishwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wengine waliohamishwa kamati za Bunge ni, Godwin Kunambi wa Mlimba mkoani Morogoro kutoka kamati ya mambo ya mambo ya nje, ulinzi na usalama kwenda kamati ya ardhi, maliasili na utalii huku Asia Halamga akiteuliwa kuwa mjumbe kamati ya masuala ya UKIMWI.

Wa mwisho kwenye mabadiliko hayo ni Agnes Marwa aliyeteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya masuala ya UKIMWI.

error: Content is protected !!