May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Msigwa: Tutatoa leseni kwa magazeti yaliyofungiwa, Kubenea atoa neno

Gerson Msigwa, Mkuu wa Idara ya Habari na Maelezo

Spread the love

 

MKURUGENZI wa Idara ya Habari-Maelezo nchini Tanzania, Gerson Msigwa amesema, wako tayari kutoa leseni kwa magazeti yote yaliyofungiwa ili yaanze kufanya kazi. Anaripoti Bupe Mwakiteleko….(endelea).

Ni baada ya Rais wa Taifa hilo, Samia Suluhu Hassan, kuagiza magazeti yote yaliyofungiwa na kumaliza adhabu zao, wapewe leseni ili waendelee na majukumu yao.

Rais Samia alitoa maagizo hayo jana Jumatatu, alipokutana na wahariri na wandishi wa habari, Ikulu ya Dar es Salaam, kuhusu siku 100 za utawala wake.

Leo Jumanne, tarehe 29 Juni 2021, Msigwa akizungumza na wahariri na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), amesema magazeti hayo yakiomba leseni yatapewa.

“Watakuja kuomba leseni na tutawapa leseni wakafanye kazi kwa kuzingatia sheria,” amesema Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania.

“Rais ametaka warudi kufanya kazi na matarajio ya serikali wafanye kazi bila kuvunja taratibu,” amesema

Msigwa ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu amesema “vikipewa leseni kazingatieni sheria na sisi si dhamira yetu na mimi ninawaahidi waandishi, sitatekeleza hili la kufungia vyombo vya habari.”

Magazeti yaliyofungiwa na kumaliza adhabu zao zaidi ya mwaka sasa ni; MwanaHALISI, Mawio na Mseto. Pia, Tanzania Daima limenyang’anywa leseni yao

Naye Mkurugenzi Mtendaji na mhariri mtendaji wa magazeti ya MwanaHALISI, Saed Kubenea amesema, “nimemsikia Rais Samia, kuhusiana na magezeti yaliyokuwa yamefungiwa. Ninamshukuru sana.”

“Nimefurahishwa na hatua yake ya kuelekeza watendaji wa serikali, kutoa leseni kwa magazeti hayo, jambo ambalo litayafanya kurejea tena mtaani. Hakika, uamuzi wake huu, kwetu umetupa faraja.”

Kubenea amesema “nimemsikia pia Mkurugezi wa Maelezo, Gerson Msigwa, naye namshukuru kwa maelezo yake, kwamba ofisi yake haitakuwa kikwazo kwenye utekelezaji wa maagizo ya rais.”

“Nami namhakikishia, tutafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu, huku tukitanguliza maslahi ya taifa,” amesema

error: Content is protected !!