Saturday , 11 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Msajili ajitosa sakata la Mdee na wenzake, aitwanga barua Chadema
Habari za SiasaTangulizi

Msajili ajitosa sakata la Mdee na wenzake, aitwanga barua Chadema

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi
Spread the love

 

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania, inadaiwa kuingilia kati maamuzi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ya kuwavua uanachama wabunge viti maalumu 19, kwa tuhuma za usaliti. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Tarehe 27 Novemba 2020, Chadema kilimfukuza Halima Mdee na wenzake 18, kwa tuhuma za usaliti kufuatia hatua yao ya kukubali kuapishwa kuwa wabunge viti maalumu, kinyume na msimamo wake wa kutowapeleka wawakilishi bungeni, kikisusia matokeo ya Uchaguzi MKuu wa 2020.

Akizungumza na wanahabari leo Jumatano, tarehe 14 Julai 2021, mkoani Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Benson Kigaila, amesema Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amewandikia barua akiwataka watoe maelezo kwa nini wamechukua hatua hiyo.

Kigaila amedai kuwa, hatua hiyo ya Jaji Mutungi kuwaandikia barua akiwataka wajieleze huku akijua kwamba Baraza Kuu la Chadema, linatarajia kuketi kwa ajili ya kujadili rufaa za wanachama hao, ina nia ovu.

“Wakati tunasubiri kikao cha baraza kuu na ili rufaa yao ipelekwe kwa mujibu wa katiba ya chama, tarehe 6 Julai 2021 msajili ametuandikia barua hii, akitutaka kama chama tuwasilishe maelezo kwake. Kitendo cha kututaka tutoe maelezo ili atoe uamuzi, anataka baraza kuu lisifanye kazi yake,” amedai Kigaila.

Mbali na Mdee, wabunge wengine waliokata rufaa kupinga kufukuzwa Chadema ni, Ester Bulaya, Esther Matiko, Nusrat Hanje, Grace Tendega, Jesca Kishoa, Agnesta Lambart, Tunza Malapo na Cecilia Pareso.

Wengine ni, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchesta Lwamlaza.

Kigaila amedai kuwa, katika barua ya msajili huyo wa vyama vya siasa, amesema amechukua hatua ya kuwaandikia barua baada ya wabunge hao kufikisha malalamiko ofisini kwake.

“Kwa nini tunasema nia hii ovu, msajili anajua hao watu wanaosema wanamlalamikia kwamba wamekata rufaa Baraza Kuu, bahati nzuri msajili anazo katiba zote, anajua kwamba kama kuna wanachama wamechukuliwa hatua za kindihamu na kamati kuu, anatakiwa kukata rufaa baraza kuu,” amesema Kigaila.

Kigaila ameongeza “ na anajua baraza kuu litafanyika mwaka huu, anataka tupeleke maelezo kuna watu hawakubaliani na kufukuzwa uanachama, yeye ni mwanasheria, ni jaji anajua kwamba huwezi kutoa maelezo kuhusu malakamiko ambayo hujayapata.”

Kigaila amesema Chadema hakitatoa maelezo kwa msajili huyo, kwa kuwa siyo chombo kinachoshughulikia rufaa za chama hicho.

Benson Kigaila, Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara

“Msajili anakujaje katikati ya chombo cha rufaa na rufaa haijashughulikiwa? Anataka tutoe maelezo kwake, tunatoa maelezo kwake kama nani, kama chombo gani? Chadema ina vyombo vyake vitakavyotumika,” amesema Kigaila na kuongeza:

“Kama kuna maelezo ya kueleza kwa nini walifukuzwa, yatapelekwa kwenye Baraza Kuu kwenye rufaa, hayatapelekwa kwa msajili kwa kuwa sio chombo cha rufaa.”

Kufuatia madai hayo, MwanaHALISI Online, imemtafuta Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sixty Nyahoza, ambaye amesema ofisi hiyo haiingilia maamuzi ya Chadema, bali inatekeleza wajibu wake wa kusimamia vyama vya siasa.

“Sisi hatuingilii maamuzi ya vyama, tunatekeleza wajibu wetu wa kusimamia Sheria ya Vyama vya Siasa na msajili anaposimamia utekelezaji wa sheria ni pamoja na kuangalia sheria inatekelezwa kwa mujibuwa wa katiba za vyama vyao,” amesema Nyahoza.

Nyahoza ameongeza “ndiyo maana tukawaambia wawasilishe maelezo, tunatekeleza kazi kwa mujibu wa sheria, tunasimamia utekelezaji wa sheria na katiba.”

Sisty Nyahoza, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Tanzania

Naibu Msajili huyo wa vyama vya siasa, amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka wa wabunge hao 19, wanaopinga hatua ya kuvuliwa uanachama wa Chadema.

Wakati huo huo, Nyahoza amehoji kwa nini Chadema kimeweka hadharani mawasiliano ya kiofisi.

“Tumepokea malalamiko, kutoka kwa wabunge wote 19. Wao wanaweza kuja hadharani kutoa mawasiliano ya kiofisi, sisi hatujaenda kuweka wazi walichotuandikia sababu hayo ni mawasiliano ya kiofisi,” amesema Nyahoza na kuongeza:

“Hatujadili mambo ya kiofisi kwenye vyombo vya habari, huwa tunaandikiana kiofisi hizi barua,” amesema Nyahoza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Vijana UVCCM Kagera wataka mwenyekiti wao ajiuzulu

Spread the loveVIJANA wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kagera wamemtaka Mwenyekiti...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina awavaa mawaziri wanaompelekea majungu Rais Samia

Spread the loveMBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) amewataka baadhi ya mawaziri...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

THRDC, Wizara ya Katiba wajadili uanzishaji haki binadamu katika biashara

Spread the loveMTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umefanya...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Sitta ang’ang’ana wanafunzi watibiwe bure, Serikali yagoma

Spread the loveMBUNGE wa Urambo, Margaret Sitta, ameishauri Serikali iweke utaratibu wanafunzi...

error: Content is protected !!