January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kikwete ataja mfupa uliomshinda akiwa madarakani

Spread the love

 

RAIS wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amesema changamoto kubwa aliyomsumbua wakati wa uongozi wake, ni watumishi wa afya kugoma kufanya kazi maeneo ya vijijini. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kikwete amesema hayo leo Jumatano, tarehe 14 Julai 2021, akizungumza katika kongamano la kumbukizi ya mwaka mmoja, tangu kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa, lililofanyika Mlimani City, mkoani Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo aliyekipokea kijiti cha urais kutoka kwa Mkapa, aliiongoza Tanzania katika kipindi cha miaka 10 mfululizo, kuanzia 2005 hadi 2015.

Kikwete amesema, licha ya Serikali kuwaajiri watumishi hao na kuwapa marupurupu yote, waligoma kufanya kazi katika maeneo hayo, kutokana na ukosefu wa miundombinu bora, hasa nyumba za kuishi.

“Moja ya changamoto nilizokutana nazo wakati wa urais wangu, ilikuwa ni kupata wataalamu wa afya kwenda kufanya kazi maeneo ya vijijini. Licha ya Serikali kuwa tayari kuwalipa mishahara na maslahi mengine, ilikuwa ngumu kuwapeleka katika maeneo hayo,” amesema Kikwete.

Kikwete ameongeza “ unawateua wanakwenda eneo walilopangiwa, kisha wanakwambia nakwenda kuchukua mizigo, harudi tena. Hii ilikuwa changamoto kubwa sana.”

Kikwete amesema kuwa, Mkapa kupitia Taasisi yake ‘Benjamin Mkapa Foundation’, alimsaidia kukabiliana na changamoto hiyo.

“Taasisi ya Mkapa ilikuja kufanya kazi na sisi ndani ya Serikali, tuliwaajiri wafanyakazi wa taasisi hiyo 1,147 tukawapeleka Tanzania Bara na Zanzibar. Tuliwachukua sababu walikuwa tayari katika maeneo husika,” amesema Kikwete.

Pia, Kikwete amesema taasisi hiyo ilisaidia kutatua changamoto ya uhaba wa makazi ya watumishi wa afya maeneo ya vijijini, kupitia miradi yake ya ujenzi wa nyumba za watumishi iliyokuwa inatelekeza.

“Shida nyingine tuliyokuwa nayo, unamchukua mtu halafu hakuna malazi. Kijana anatoka chuoni anakwenda kule tafuta tafuta utakaa wapi, anakuta baadhi yake ni nyumba za matembe. Wanasema sawa nakuja ngoja nikajipange, kisha harudi tena,” amesema Kikwete.

Mkapa aliyezaliwa tarehe 12 Novemba 1938, alifariki dunia tarehe 24 Julai 2020 na kuzikwa nyumbani kwao Lupaso mkoani Mtwara, tarehe 29 Julai mwaka jana.

Enzi za uhai wake, Mkapa aliiongoza Tanzania kuanzia 1995 hadi 2005. Baada ya kuondoka madarakani, Tarehe 13 Aprili 2006, alianzisha taasisi hiyo.

error: Content is protected !!