December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mifumo ya Afya yatakiwa kuandikwa kwa kiswahili kusaidia wananchi

Spread the love

KATIBU  Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainabu Chaula amewagiza wataalamu wa sekta ya Afya wanaohusika katika kutengeneza nifumo ya takwimu iandaliwe kwa lugha ya kiswahili. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mbali na kutaka mifumo ya takwimu katika sekta ya afya kutumiwa kwa kiswahili amesema kuwa itaondoa changamoto ya kutoelewa vyema mfumo wa takwimu kutokana na kutumiwa kwa lugha ya kigeni.

Dk. Chaula alisema hayo wakati anafunga Kongamano la Tatu la Wataalamu wa Afya, ambalo hufanyika kila mwaka baada ya kuasisiwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe.

“Hata kongamano la mwaka jana tulijadili matumizi ya takwimu kuanzia ngazi za msingi mpaka juu, lakini mambo hayaendi tena kwenye ngazi za msingi ndiyo mtihani kweli kweli, mtihani huu unaletwa na wadau wanaoleta fedha zinazotuvuruga,” amesema Dk. Chaula

Amesema mifumo itengenezwe kwa kiswahili, kwa sababu ni lugha rafiki kwa wanaotakiwa kuitumia na  ikiwa wadau wanataka lugha tofauti na hiyo, watengenezewe mifumo yakwao kwa lugha wanayotaka.

Dk.Chaula amesema hatua hiyo itawezesha kila kada kufahamu kinachofanyika kwenye kada nyingine, tofauti na sasa ambapo licha ya Nchi kuwa na wataalamu wengi kila mmoja anapita njia yake.

Kwa upande wake aliyewahi kushika nafasi ya Uwaziri wa Wizara ya Afya katika serikali ya awamu ya Nne, Dk. Rashid Seif, amesema sekta ya afya ina jumla ya mifumo 160, hali inayodhihirisha kila mmoja alikuwa akitengeneza mfumo kulingana na uhitaji wake, mahali anakofanyia kazi, upungufu au uhitaji aliyokuwa nao.

Amesema kwasasa wanaangalia mifumo inayofaa kubaki, iboreshwe ili huduma kwa mgonjwa ziboreke.

Kwa mujibu wake, mifumo hiyo inatakiwa kuhusisha mambo yote ikiwemo inayoonesha mapato ikiwa yanaongezeka, yanashuka pamoja na ile inayoonesha ikiwa kuvuja kwa mapato kumedhibitiwa.

“Kuna baadhi ya hospitali japo ni chache zipo computorised (zenye mifumo ya kielektroniki) , mgonjwa anaingia mpaka anatoka hana karatasi hata moja,” amesema Dk. Rashid.

Naye Mkurugezi Msaidizi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Dkt. Anna Nswila, amesema data zinapotafutwa kwa wakati na kuchambuliwa vizuri na zikatumiwa kwa ukamilifu, hutoa matokeo yenye tija.

Amesikitishwa na wataalamu wasiyotumia takwimu, akisema wataalamu hao wanafanya upasuaji wa miili ya binadamu na kurekebisha viungo mbalimbali, ikiwemo mifumo ya fahamu na kuhoji inakuwaje washindwe kutumia mifumo ya taarifa zinazohusu kazi zao za kila siku?

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Skuli ya Utawala  wa Umma na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Eliza Mwakasangula, akitoa taarifa na tathmini ya kongamano pamoja na maombi kwa serikali amesema, mwaka huu washiriki wamepungua ikilinganishwa na mwaka jana.

Baadhi ya Wataalamu wa Afya wameiomba  serikali kuendelee kushirikiana na chuo hicho kuandaa kongamano hilo kila mwaka, pamoja na kuwahimiza  watendaji katika halmashauri na mikoa, kutenga bajeti ya fedha ili nao wawe washiriki kongamano hilo.

error: Content is protected !!